1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Wapalestina 15 wauawa na jeshi la Israel huko Gaza

20 Novemba 2024

Vikosi vya Israel vimewaua Wapalestina 15 leo kwenye Ukanda wa Gaza, akiwemo mfanyakazi mmoja wa idara za uokozi, huku vifaru vya kijeshi vikiendelea kupiga doria kote kwenye eneo hilo na kulipua majengo ya maakazi.

https://p.dw.com/p/4nCDH
Ukanda wa Gaza | Israel | Bait Lahia
Watu wakiangalia vifusi vya jengo lililoharibiwa kufuatia shambulio la anga la Israel huko Beit Lahya kaskazini mwa Ukanda wa GazaPicha: -/AFP

Vikosi vya Israel vimewaua Wapalestina 15 leo kwenye Ukanda wa Gaza, akiwemo mfanyakazi mmoja wa idara za uokozi, huku vifaru vya kijeshi vikiendelea kupiga doria kote kwenye eneo hilo na kulipua majengo ya maakazi.

Hayo yameelezwa na wakaazi pamoja na maafisa wa afya wa ukanda huo unaodhibitiwa na kundi la wanamgambo wa Hamas. Matabibu wamesema watu wasiopungua 12 wameuwawa baada ya Israel kuishambulia nyumba moja kwenye eneo la Jabalia, kaskazini mwa Gaza na kwamba watu wengine 10 bado hawajapatikana na kazi ya kuwatafuta inaendelea.

Soma pia: Mashambulizi ya Israel yamuua afisa mawasiliano wa Hezbollah 

Kwenye kitongoji cha Sabra, Idara ya Huduma za Dharura imesema mfanyakazi wake mmoja ameuawa kufuatia shambulizi la anga la Israel lililoulenga msafara wao.

Wakaazi wa maeneo ya Jabalia, Beit Lahiya na Beit Hanoun, ambako jeshi la Israel linaendesha operesheni zake tangu mwezi uliopita, wamearifu kwamba vikosi hivyo vimeripua nyumba kadha kwenye maeneo matatu.