1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapakistan wana wasiwasi pindi Wamarekani wataondoka Afghanistan

Miraji Othman20 Novemba 2009

Jee Wamarekani wataondoka Afghanistan kwa pupa?

https://p.dw.com/p/Kc5i
Jeshi la Pakistan likijitayarisha kushambulia vituo vya Wataliban wa Pakistan katika eneo la Waziristan ya KusiniPicha: AP

Huku Marekani ikitafakari juu ya mkakati wake mpya kuelekea vita vya Afghanistan, Pakistan inangoja kwa wasiwasi. Ina wahaka kwamba kuengezeka hujuma za majeshi ya Kimarekani kutavipanua vita hivyo, lakini, wakati huo huo, ina hamu ya kuona kwamba nia ya kweli ya Marekani ya kuviendeleza vita hivyo itawashawishi Wataliban wakubali kufanya mazungumzo.

Katikati ya wiki hii, Rais Barack Obama wa Marekani aliahidi kuvimaliza Vita vya Afghanistan kabla hajaondoka madarakani. Alisema atatangaza karibuni matokeo ya uchunguzi wake uliongojewa kwa muda mrefu, na utakuwa pamoja na mkakati wa kuyaondoka majeshi ya Kimarekani kutoka Afghanistan ili kuepuka kukaliwa nchi hiyo kwa miaka mingi, jambao ambalo alisema halitasaidia maslahi ya Marekani. Kuna karibu wanajeshi wa kigeni 110,000 katika Afghanistan, wakiwemo 68,000 wa Kimarekani, nusu yao wamewasili huko tangu Rais Obama akamate madaraka. Hivi sasa rais huyo yuko katika mchakato wa kufikia uamuzi kama ayakubalie maombi yaliotolewa na makamanda wake wa kijeshi wanaotaka maelfu zaidi ya majeshi yapelekwe Afghanistan.

Hofu hizo zilizushwa hivi karibuni mjini Islamabad kwa mshauri wa Kimarekani wa masuala ya usalama wa taifa, Jenerali James Jones. Afisa mmoja wa Pakistan alisema wao wana hofu kwamba Wataliban huenda watajaribu kuvuka mpaka na kuingia Pakistan, pindi michafuko itazidi baada ya Marekani kupeleka wanajeshi wepya. Hali hiyo, bila ya shaka, itafanya mambo yawe magumu zaidi kwa Pakistan, hasa katika wakati huu ambapo majeshi ya serekali ya nchi hiyo yanafanya mashambulio katika jimbo la Waziristan ya Kusini, kwenye mpaka na Afghanistan. Jeshi hilo limechukuwa vituo vikubwa muhimu vya Wataaliban katika eneo hilo la milima. Wapiganaji wa Kitaliban wamelipiza kwa kuripuwa mabomu katika miji ya Pakistan.

Wakijibu juu ya wasiwasi huo ulioelezewa na Pakistan kwamba vita vya Afghanistan vinaweza vikasambaa na kuingia Pakistan, maofisa wa Kimarekani wanasema majeshi mepya hayatafungua medani mpya za mapigano, lakini yatajishughulisha kuyaweka maeneo yaliosheheni raia kuwa ya usalama zaidi.

Wakati ikiwa na wasiwasi juu ya kuwasili majeshi mepya ya Kimarekani huko Afghanistan, Pakistan ina wasiwasi zaidi juu ya uwezekano wa kuondoka majeshi hayo. Bado ingali inakumbukwa huko Pakistan namna Marekani ilivojitenga kutoka Afghanistan baada ya Warussi kuondoka huko mwaka 1989 na kuiwacha nchi hiyo katika vurugu. Mchunguzi mmoja wa zamani wa Shirika la Upelelezi la Marekani, CIA, Bruce Riedel, anasema Wapakistani wanahisi Marekani itakimbia, na wao wataachiwa uchafu utakaobaki, kama walivoachiwa uchafu katika miaka ya tisini.

Mazungumzo ya Barack Obama kwamba majeshi ya Marekani yataondoka Afghanistan kabla yeye hajaacha urais yanazidisha hofu hizo kwamba Marekani itakimbilia kuondoka. Barack Obama atamaliza muhula wake wa kwanza wa utawala miaka mitatu kutoka sasa. Vipindi viwili vya utawala wake vitamalizika miaka saba kutoka sasa. Pakistan inataka Marekani iondoke Afghanistan kwa utaratibu wenye nidhamu, na baada ya kupatikana suluhisho kwa njia ya mazungumzo litakalowaingiza pia badhi ya Wataliban. Wataliban wataiona ishara yeyote ya kutia na kutoa kutoka kwa Marekani kuwa ni udhaifu, na watasukumwa tu kufanya mashauriano ikiwa watakuwa na uhakika kwamba yako majeshi nyuma ya nia ya Marekani.

Marekani, wakati huo huo, inaitaka Pakistan iwe kama wakala wa kufanya mazungumzo na Wataliban. Pakistan ilivunja rasmi maingiliano yake na Wataliban wa Afghanistan baada ya kufanyika yale mashambulio ya Septemba 11 huko Marekani.

Mwandishi: Miraji Othman/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdulrahman