Wanawake washiriki mafunzo ya Kampeni Tanzania.
22 Juni 2015Mmoja wa Wanasiasa anayechipukia Asha Salum anakazi ya kujaribu kuwashawishi watu katika eneo lake la Dar Es Salaam kumuunga mkono kugombea nafasi ya udiwani katika uchaguzi ujao mwaka huu, na anaongeza idadi ya wanawake wanaotafuta ofisi ya kisiasa nchini Tanzania.
Mwanasiasa huyo mpole, ambaye ana umri wa miaka 31 ni Mgombea mdogo katika nafasi ya udiwani katika jimbo la uchaguzi la Tegeta lililopo Kawe katika kipindi cha miaka 20, ni mmoja wa wanawake wa kizazi kipya ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuingia katika uwanja wa siasa ambao umezoeleka kudhibitiwa na wanaume.
Taifa hilo la Afrika Mashariki lenye watu wapatao milioni 50 limekuwa na wanawake wachache katika nafasi ya juu ya uongozi tangu kupitishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 lakini wanaharakati wanawake wana matumaini ya kuwepo na mabadiliko katika awamu ya tano ya uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Salum ni moja kati ya wanasiasa wanawake wanaochipukia 2,600 ambao manapata mafunzo ambayo yalianza wiki hii kutoka muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nchini Tanzania kuhusu namna ya kuboresha ujuzi wa kufanya kampeni na kuepuka mitego ya ngono ambayo inawakabili mara nyingi wanawake wa Kitanzania katika juhudi za kuendeleza kazi zao.
Mafunzo, yaliandaliwa na Umoja wa wanawake wanasiasa nchini Tanzania (TWCP), yana lengo la kuwapatia wagombea wanawake wanaogombea mwezi Oktoba urais, ubunge na udiwani ujuzi na mbinu za kisiasa.
Kwa mujibu wa waandaaji wa mafunzo, wagombea watapata mafunzo kuhusu mada za masuala ya kisiasa yanayozunguka uchaguzi, jukumu la bunge na mabaraza ya mitaa, na umuhimu wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.
Wanawake katika nyadhifa za kisiasa Tanzania
Wagombea wanne wanawake wameonyesha nia katika mbio za kuwania urais kupitia tiketi ya CCM, ikiwa ni pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Asha -Rose Migiro.
Hii ni mara ya kwanza nchini Tanzania wanawake kujitokeza kutafuta uteuzi katika nafasi ya urais.
Migiro, ni mwanasheria kitaaluma, alifanya kazi katika Umoja wa Mataifa chini ya Ban Ki-moon kuanzia 2007-2012 na amekuwa mtu wa 12 katika mawaziri Tanzania kueleza nia yake ya kutaka kuwa mrithi wa Rais Jakaya Kikwete ambaye anamaliza muda wake baadaye mwaka huu.
Tanzania imejaribu kuhakikisha uwakilishi wa wanawake kupitia mfumo wa asilimia 30 ya viti maalumu bungeni katika jumla ya viti 357. Vyama vya siasa vinavyopata angalau asilimia 5 ya kura kwenye uchaguzi mkuu kuteua wanawake kwa nafasi hizo.
Lakini Wanakampeni wa haki za wanawake wana wasiwasi juu ya wingi wanawake bungeni unatokana na viti maalum na si kuchaguliwa moja kwa moja kutoka kwenye majimbo.
Wanakampeni wana wasiwasi kutokana na wanawake kutokuwa na ujuzi,elimu na uzoefu ambao utawawezesha kufikia mafanikio katika siasa na wengi hawana fedha za kutosha za kuwawezesha kwenye siasa zaidi ya fedha kidogo za mahitaji ya msingi ya familia.
Ingawa idadi ya wabunge wanawake imeongezeka kufikia asilimia 35 katika uchaguzi 2010 kutoka asilimia 21.5 mwaka 2000, makundi ya haki yanasema haitoshi kutokana wanawake 17 tu walichaguliwa kutoka majimbo ya uchaguzi.
Pamoja na changamoto, ushiriki wa wanawake katika siasa
umeongezeka katika nchi nyingi za Afrika katika miongo miwili iliyopita.
Malawi hivi karibuni walikuwa na rais wa kwanza mwanamke, Joyce Banda, na rais wa Liberia Ellen Johnson Sirleaf ambaye alichukuwa ofisi ya juu ya nchi yake tangu mwaka 2006.
Rwanda inaongoza duniani kwa kuwa na asilimia 63.8 ya viti vya wabunge wanawake, kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa.
Mwandishi:Salma Mkalibala/RTRE
Mhariri:Josephat Charo