1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake washambuliwa kingono mwaka mpya Cologne

5 Januari 2016

Karibu wanaume 1,000 wanadaiwa kuwafanyia dhuluma za kingono wanawake katika mkesha wa mwaka mpya katika mji wa magharibi mwa Ujerumani wa Cologne, katika uhalifu uliyowaacha viongozi wakiwa na mfadhaiko.

https://p.dw.com/p/1HY20
Kituo kikuu cha treni cha mjini Cologne, ambako uhalifu unadaiwa kutendeka.
Kituo kikuu cha treni cha mjini Cologne, ambako uhalifu unadaiwa kutendeka.Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Polisi ya Ujerumani imeyaelezea mashambulizi hayo ya kingono dhidi ya wanawake kama mwelekeo mpya kabisa wa uhalifu, baada ya kupokea malalamiko karibu 60 ya jinai, likiwemo moja la madai ya ubakaji.

Wanawake walisema walidhalilishwa na kundi la wanaume waliokuwa wamekusanyika katika uwanja ulioko kati ya kituo kikuu cha treni cha mji huo na kanisa kuu la Gothic, huku maafisa wakisema wanatarajia waathiriwa zaidi watajitokeza katika siku zijazo.

Mkuu wa jeshi la polisi mjini Cologne Wolfgang Albers alisema mashahidi waliayalezea mashambulizi hayo kuwa yalitokea kwa kundi la wanaume waliofikia 1,000, ambao muonekano wao ulionyesha wana asili ya Kiarabu au kutoka Afrika Kaskazini.

Meya wa jiji la Cologne Henriette Reker.
Meya wa jiji la Cologne Henriette Reker.Picha: picture-alliance/dpa/R. Vennenbernd

Mkuu huyo wa polisi ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa, kwamba matukio hayo yanawakilisha kile alichokiita "hali isiyokubalika kwa mji wa Cologne, na idara yake tayari imeunda kikosi kazi kushughulikia suala hilo.

Meya aitisha mkutano wa dharura

Meya wa jiji la Cologne Henriette Reker, ambaye alipamba vichwa vya habari za kimataifa mwezi Oktoba baada ya kuchomwa kisu wakati akiwa kwenye kampeni, ameitisha mkutano wa dharura siku ya Jumanne, ambao unawahusisha maafisa wa polisi wa ndani na wa shirikisho kujadili uhalifu huo.

Reker aliwaambia waandishi wa habari kwamba vitendo vya wanaume hao vilikuwa vya kinyama, na kuongeza katika mahojiano na gazeti la Kölner Stadt-Anzeiger, kwamba hawawezi kuvumilia uvunjifu huu wa sheria.

Akizungumza na gazeti la mjini Bonn la Express, waziri wa mambo ya ndani wa jimbo la North Rhine-Westphalia Ralf Jäger, aliahidi kuchukuwa hatua za haraka.

Madhara yasiyofurahisha ya kisiasa

Mkuu wa tawi la North Rhine-Westphalia la chama cha watumishi wa jeshi la polisi nchini Ujerumani GdP, Anold Plickert, aliutaja uhalifu huo kuwa ni shambulizi kubwa dhidi ya haki za msingi, na kusema haki laazima itendeke hata kama itakuwa na madhara yasiyofurahisha ya kisiasa. Plickert alionya hata hivyo, dhidi ya kulitumia tukio hilo kuchochea hisia za chuki dhidi ya wakimbizi.

Polisi wakisimamia usalama mbele ya kituo kikuu cha treni mjini Cologne siku ya mkesha wa mwaka mpya.
Polisi wakisimamia usalama mbele ya kituo kikuu cha treni mjini Cologne katika mkesha wa mwaka mpya.Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Alisema mkimbizi yeyote mwenye tatizo la kujumuika katika jamii yetu iliyo wazi na kuheshimu haki za watu wengine, anapaswa kushughulikiwa kwa kutumia nguvu kamili ya sheria, lakini akaongeza kuwa umma haupaswi kusahau kuwa idadi kubwa ya watu waliokuja Ujerumani wamefanya hivyo kwa sababu maisha yao hayako salama tena katika mataifa yao.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/ape/DW

Mhariri: Caro Robi