Wanawake wa Somalia mashakani
21 Januari 2011Hivi karibuni, Al-Shabbaab walitoa agizo kwa wanawake wanaoshi katika mji wa Kismayu kutofanya biashara za kubadilishana na wanaume wanaofanya kazi kwenye meli zinazotia nanga katika bandari ya pwani ya mji huo.
Wamewakataza pia kushikana mikono na wanaume mbele za watu, wamewaka kusafiri peke yao, na hawawaruhusu kufanya biashara yoyote wala kufanya kazi ofisini.
Kiongozi wa juu wa Al-Shabbaab amesema kuwa mwanamke hatakiwi kuonekana yupo na mwanaume kutoka nchi nyingine katika eneo la bandari, na yeyote atakayekwenda kinyume na agizo hili, atakamatwa.
Al-Shabbaab wapiga marufuku muziki, sinema
Neno Al-Shabbaab lina maana ya kijana katika lugha ya Kiarabu, lakini kundi hili limepiga marufuku mambo yote yanayopendelewa na vijana. Kwa mfano, limepiga marufuku kuangalia sinema, miziki inayosikika katika milio ya simu, kucheza ngoma kwenye sherehe za harusi na kuangilia mpira kwenye televesheni.
Wanawake wengi katika mji wa Kismayu ni wajane, kwa ama kuachika au kufiliwa na waume zao. Wameishi kwa miaka kadhaa kwa kutegemea biashara ya kubadilisha mboga za majani na matunda, na kupewa mafuta na bidhaa zingine kutoka kwa wafanyakazi melini.
Akiongea kwa simu na Shirika la Habari la Reuters, Hawa Olow, alisema kuwa, yeye ana watoto watatu na amewakuza kwa hicho kidogo anachokipata kupitia biashara ya kubadilishana bidhaa bandarini, lakini kwa sasa hawezi tena kufanya biashara hiyo.
Al-Shabbaab wameamuru wanawake lazima wanunue na wavae vazi maalum refu na pana, ambao kundi hilo linatengeneza.
Vile vile, wanamgambo hawa wamepiga pia marufuku biashara ya mirungi inayotafunwa sana na wanaume na kulewesha kiasi. Mirungi maarufu sana katika nchi hiyo ya pembe ya Afrika. Wanawake wengi katika mji wa Kismayu hujishughulisha pia na biashara hii kwa magendo, lakini wakikamatwa wanafungwa jela siku 20 na kulipa faini ya shilingi milioni moja za Kisomali.
Mwanamke mwengine, ambaye hufanya biasahra hiyo, ameimbia Reuters kuwa, wakati wa vita walikuwa na maisha mazuri na amani kidogo, lakini sasa hali ya maisha ni ngumu kwa kuwa utawala wa Al-Shabbaab unatoa adhabu kali hata kwa vitu vidogo vidogo.
Mwanamke huyo amesema Al-Shabbaab wamewaambia wanawake hawatakiwi kufanya shughuli yoyote ile.
"Kwa kuwa wengi wa wanawake hawana waume, wameachika au waume zao wamekufa kutokana na mapigano, maisha kwa ujumla yamevurugika." Anasema mwanamke huyo.
Mwanamke haruhusiwi kukaa karibu na mwanamme katika basi na akisafiri lazima asindikizwe na mwanaume mwenye undugu naye.
Profesa wa Historia katika Chuo Kikuu cha Nairobi nchini Kenya, Abdiwahab Abdi-Samad, anasema katika familia yake wamezaliwa na kukua wakiwa Waislamu na haoni mahala palipoandikwa katika Uislamu mwanamke asifanye kazi. Anasema wanachofanya Al- Shabbaab ni kuchukua nadharia hizo kutoka kwa kundi la Taliban la nchini Afghanistan na wanamgambo wengine wenye itikadi kali.
"Ikiwa Al-Shabbaab hawataki wanawake wafanye kazi, basi lazima wawape pesa ili familia zinazowategemea ziweze kuishi." Anasema Profesa Abdi-Samad.
Katika mji wa Afgoye, uliopo kusini mwa mji mkuu wa Mogadishu, ambako Bibi Fatuma Ahmed anaishi, amesema yeye mwenyewe alichapwa bakora mbele za watu na kijana mdogo anayelingana na mjukuu wake kwa kutovaa vazi lililoamriwa na Al-Shabbaab.
Bibi Fatuma ameambiwa asivae nguo zake za zamani, lakini anasema yeye ni mzee wa zaidi ya miaka 60, hivyo hakuna hata mwanamme anayemtupia macho.
"Kwa nini wananilazimisha nivae nguo hizi nzito?" Anauliza kwa uchungu Bi Fatma.
Mwandishi: Fatuma Matulanga/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman