Wanawake wa Saudi Arabia waruhusiwa kuingia uwanjani
12 Januari 2018Hata hivyo wanawake leo wanaruhusiwa kutazama mchuano huo wakikaa katika sehemu tafauti na wanaume.
Ili kujiandaa na mabadiliko hayo, Saudi Arabia imeunda kile kinachojulikana kama sehemu za familia katika viwanja vya michezo kwa ajili ya wanawake, zikitenganishwa na vizuwizi kutoka maeneo yanayokaliwa na wanaume pekee. Viwanja hivyo vimewekewa pia maeneo ya kuswali kwa ajili ya wanawake pekee, maeneo ya kupumzika na kuvuta sigara, na pia milango tofauti ya kuingilia na maegesho ya magari makhsusi kwa watazamaji wa kike.
Ni ushindi mwengine kwa wanawake wa Saudi Arabia kwani kwa mara ya kwanza watapata fursa ya kushuhudia mpambano kati ya timu mbili za ndani ambazo ni klabu za ligi kuu ya Saudi Arabia Al Ahli na Al Batin.
Wakati wengi wamekaribisha uamuzi huo, baadhi ya wameukosoa. Hashtag ya Kiarabu kuhusu wanawake kuingia viwanja vya michezo ilipata tweet zaidi ya elfu 50 kufikia majira ya mchana. Wengi walitumia hashtag hiyo kuandika kwamba nafasi ya wanawake inapaswa kuwa nyumbani, wakielekeza juhudi zao katika kuwaangalia watoto na kuhifadhi imani zao, na siyo uwanjani ambako mashabiki hulaani mara kwa mara na kutamka maneno mazito.
Mrithi wa kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia, Mwanamfalme Mohammed bin Salman mwenye umri wa miaka 32, mtoto wa Mfalme Salman na mrithi wake, anaangaliwa kama mtu alie nyuma ya mabadiliko haya yote. Anatazamiwa kurithi taifa ambako zaidi ya nusu ya wakaazi wana umri wa chini ya miaka 25 na wenye shauku ya mabadiliko.
Badala ya kuwapa raia haki zaidi za kisiasa, mrithi huyo wa ufalme amejikita zaidi katika kuimarisha umaarufu wake kwa kuzuwia ushawishi wa wahafidhina. Mageuzi yake pia yanalenga kwa sehemu, kuongeza matumizi ya raia kwenye burudani, mnamo wakati taifa hilo likikabiliwa na miaka kadhaa ya nakisi ya bajeti inayotokana na kushuka kwa bei za mafuta.
Uwanja wa kwanza kuwapokea wanawake utakuwa katika mji wa bahari ya Sham wa Jeddah, kuhudhuria mechi hiyo kati ya Al-Ahli na Al-Batin jioni ya leo. Uwanja wa taifa mjini Riyadh, utafungua milango yake kwa wanawake kesho Jumamosi, ukifuatiwa na mji wa magahribi wa Dammam Alhamisi wiki ijayo.
Viwanja hivi vilijengwa kwa mamilioni ya dola wakati bei za mafuta zikiwa karibu mara mbili ya bei za sasa. Serikali ilitumia fedha nyingi kwenye viwanja hivyo katika juhudi za kuwaridhisha vijana wa Kisaudi, na kutoa fursa kwa mashabiki wenye shauku ya kuzipa motisha timu za ndani, na pia kwa ajili ya magwaride na sherehe za kitaifa.
Katika tukio la mara moja, uwanja mkuu wa mjini Riyadhi uliwaruhusu wanawake kuingia kutazama shughuli za siku kuu ya taifa mwezi Novemba, hii ikiwa ndiyo mara ya kwanza kwa wanawake kutia mguu ndani ya uwanja wa taifa, ingawa wanawake raia wa kigeni wamekuwa wakiruhusiwa kuingia viwanjani tangu miaka kadhaa iliyopita.
Mwandishi: Fathiya Omar
Mhariri: Saumu Yusuf