1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yatumia wanawake wa Kiafrika kutengeneza droni

Angela Mdungu
10 Oktoba 2024

Karibu wanawake 200 wenye miaka 18-22 kutoka barani Afrika, wamekuwa wakisajiliwa kwenda kufanya kazi Urusi, katika kiwanda kinachohusika kuunda maelfu ya droni za Iran zinazotumika kuishambulia Ukraine.

https://p.dw.com/p/4lcOQ
Ndege isiyo na rubani ya Iran aina ya Shahed
Droni aina ya Shahed ya IranPicha: Sobhan Farajvan/Pacific Press/picture alliance

Karibu wanawake 200 wenye miaka 18-22 kutoka barani Afrika, wamekuwa wakisajiliwa kwenda kufanya kazi Urusi, katika kiwanda kinachohusika kuunda maelfu ya droni za Iran zinazotumika kuishambulia Ukraine. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti maalumu iliyotolewa na shirika la habari la Associated Press baada ya kukamilisha uchunguzi wake.

Wanawake hao kutoka barani Afrika wamekuwa wakifanya kazi kwenye kiwanda cha droni sambamba na wanafunzi wa vyuo vya ufundi wa Urusi. Katika mahojiano ya shirika la habari la AP baadhi ya wanawake wamesema walilaghaiwa kuwa wangekwenda Urusi katika programu ya kufanya kazi na kusoma. Badala yake wameeleza kwamba wamekuwa wakifanya kazi kwa muda mrefu huku wakifuatiliwa muda wote.

Wamekutana na ahadi hewa kuhusu kiasi cha mishahara na programu za mafunzo huku wakifanya kazi zinazohusisha kemikali ambazo zimewasababishia athari katika ngozi zao.

Soma zaidi: Mataifa ya magharibi yaiweka vikwazo Iran upelekaji silaha Urusi

Kulingana na shirika la habari la The Associated Press, lilifanya uchambuzi wa picha za satelaiti za jengo lililo katika eneo la Urusi linalofahamika kama Jamhuri ya Tatarstan sambamba na nyaraka za ndani zilizovuja. Pia lilipata mamia ya video zilizo katika programu ya usajili ya mtandaoni na kufanikiwa kufahamu maisha katika kiwanda kilicho katika kile kinachoitwa Kanda maalumu ya Uchumi ya Alabuga, kilometa 1,000 mashariki mwa Moscow.

Ripoti ya shirika hilo la habari imebainisha kuwa, Urusi inayokabiliwa na uhaba wa nguvukazi katika kipindi hiki cha vita kupitia Abaluga, imewaajiri wanawake hao ambao ni kutoka nchi za Uganda, Rwanda, Kenya, Sudan Kusini, Sierra Leone na Nigeria, pamoja na Sri Lanka iliyo Kusini mwa bara la Asia.

Urusi inapanga kutengeneza droni 6,000 kwa mwaka

Taarifa ya shirika la habari la AP imebaini kuwa Urusi inapanga kutengeneza droni 6,000 kwa mwaka. Nchi hiyo na Iran zilitia saini mkataba wenye thamani ya dola za Kimarekani bilioni 1.7 baada ya Rais Vladmir Putin kuanza uvamizi katika taifa jirani la Ukraine. Moscow ilianza kuingiza droni za Iran mwaka mmoja baadaye.

Vladmir Putin
Rais wa Urusi Vladmir PutinPicha: Sputnik/Gavriil Grigorov/Pool via REUTERS

Aliyekuwa mkaguzi wa silaha wa Umoja wa Mataifa David Albright ambaye kwa sasa ni mtaalamu katika taasisi ya Sayansi na Usalama wa Kimataifa amesema kuwa karibu asilimia 90 ya wanawake kutoka mataifa ya kigeni walioajiriwa kupitia kampeni iliyoitwa "Alabuga start"  wanafanya shughuli ya kuunda droni.

Soma zaidi: Iran yalaaniwa vikali katika kura ya Baraza la Usalama

Kwa mujibu wa mmoja wa wafanyakazi hao wa kigeni, husafiri kwa mabasi kutoka kwenye mahali wanapoishi kwenda kiwandani huku wakipitia vituo kadhaa vya ukaguzi. Wanachangia vyumba vya kuishi na majiko katika eneo ambalo linalindwa saa 24.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Urusi yamesema hayafahamu juu ya kilichokuwa kikiendelea kwenye kiwanda hicho ingawa wanakiri kuwa taarifa hizo zinaendana na hatua zinazochukuliwa na Urusi katika kupata wafanyakazi.