1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wako nchini Ujeruman wakipatiwa matibabu

25 Agosti 2016

Wanawake na wasichana 1,1000 wa kabila la Yazidi kaskazini mwa Iraq ambao ni wahanga wa vitendo vya ubakaji na unyanyasaji vilivyofanywa na wapiganaji wa kundi IS2014 wako nchini Ujerumani wakipatiwa msaada na matibabu

https://p.dw.com/p/1JpOZ
Askari wa kike wa Kikurdi akiwa na wenzie wakijiandaa na mapambano dhidi ISPicha: Reuters/A. Jadallah

Wengi wa wanawake na wasichana wa kabila hilo walitekwa na wapiganaji wa IS kwa takribani mwaka mzima, ambamo ndani ya kipindi hicho walikuwa wakibakwa, kudhalilishwa na kutumikishwa kazi za sulubu, kuku wengi wengine wakiuzwa utumwani, na wale wa kiume wakilazimishwa kujiunga na kundi hilo na wanaume wazee kuuwawa iwapo walikataa kubadili dini na kuwa Waislamu.

Baada ya uvamizi huo, maelfu ya watu walikimbilia milimani walikozingirwa na wapiganaji hao ambapo Marekani, Uingereza, Iraq, Ufaransa na Australia walitoa misada kuwasaidia, lakini wengi wao walifariki kabla ya kuokolewa.

Kufuatia tukio hilo, hakuna tena mtu wa kabila ya Yazidi anayeishi katika mkoa wa Sinjar wengi wakiwa wamepoteza maisha, wengine kuuzwa utumwani na wengine wakiwa ni wale wasiotaka kurudi tena katika eneo hilo kwa hofu ya kuvamiwa tena.

Jasmin, msichana mwenye umri wa miaka 18, ni mmoja kati ya watu waliofanikiwa kutoroka, utumwani baada ya kubakwa na kudhalilishwa kwa muda mrefu na baadaye kupelekwa katika kambi ya wakimbizi nchini Iraq.

Akiwa kituoni hapo, alikutana na daktari Jan Kizilhan ambaye kwa mara ya kwanza alipomuona hakujua kama ni daktari na hivyo kupatwa na wasiwasi kuwa pengine alikuwa ni mmoja wa wapiganaji wa kundi la IS.

Mwaka mmoja uliopita, alikaribia kujiua kwa kujimwagia mafuta ya taa na kisha kujiwasha kwa kiberiti. Kutokana na kile alichopitia, hakuona tena sababu ya kuendelea kuishi. Moto huo uliomuunguza sehemu ya nywele, puani, mdomoni na kwenye masikio na kumuacha akiwa na majeraha katika mwili wake.

Irak Nawaran Anti-IS-Miliz Frauen Kurdinnen Jesidinnen
Mpiganaji wa kabila la Yazidi akiwa katika chumba Karibu na eneo la mapigano dhidi ya ISPicha: Reuters/A. Jadallah

Jasmin anakumbuka siku ya kwanza aliyoulizwa na Daktari Jan kama yuko tayari kuelekea Ujerumani ambako angelipatiwa msaada, alisema "Ndio niko tayari, nahitaji kwenda huko ili niwe salama na nirejee kuwa yule Jasmin wa zamani." Lakini Jasmin aliomba kutokutumika kwa jina lake la pili akiwa Ujerumani kuhofia kutambulika na wapiganaji wa IS.

Ujeruman yaamua kuwasadia waathirika hao

Bunge la Ujerumani limetenga bajeti ya euro 95 milioni sawa na dola 107 za Kimarekani ili kusaidia waathirika hao na kuongeza kuwa watakapopona wanaruhusiwa kurejea nchini mwao japo wanaweza kuendelea kuishi Ujerumani ikiwa watapenda.

Mmoja kati ya wataalamu wa masuala ya saikolojia aliyetembea kambi hiyo na kukutana na msichana wa miaka 8 ambaye amebakwa mara 100 ndani ya kipindi cha miezi 10 anasema

"Huu ni unyama ambao sijawahi kuuona maishani. Mimi ni mtaalamu wa masuala ya saikolojia, nimekutana na watu wagonjwa kutoka Rwanda na Bosnia, ila hawa ni tofauti".

Wanawake na wasichana hao wanatibiwa katika vituo zaidi ya 20 katika maeneo mengine ambayo hayatakiwi kujulikana na yenye ulinzi mkali kwa hofu kuwa IS wanaweza kuelekeza mashambulizi nchini Ujerumani.

Licha ya kuwa wengi wa wanawake hao bado hawana ujasiri wa kuongelea kilichotokea, Jasmin anasema yeye yuko tayari kuzungumza akiwa na matumaini ya kuanza maisha mapya baadaye.

Mwandishi: Celina Mwakabwale/AP

Mhariri: Mohammed Khelef