1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake na changamoto kilimo cha mpunga

Admin.WagnerD3 Desemba 2013

Wanawake, kundi ambalo linaelezwa kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kuzalisha zao la mpunga Afrika wanatumia vifaa duni vya kufanyia kazi ikilinganishwa na wanaume na hivyo kujikuta wakirudi nyuma katika maendeleo.

https://p.dw.com/p/1ASTY
Matumizi ya Tekknolojia kwa wanawake ni tatizo.
Matumizi ya Tekknolojia kwa wanawake ni tatizo.Picha: Getty Images

Kwa zaidi ya miaka 20,sasa, Anastazia Ngwaun kutoka katika kijiji cha Bamunkumbit nchini Cameroon amekuwa akilima zao hilo huku akikabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwemo kulima kwa kutumia jembe la mkono na anaamini angekuwa mwanaume ingekuwa rahisi kwake kuifikia teknolojia ambayo ingemrahisishia kufanya kazi hiyo haraka.

Kilimo cha mpunga ni kazi ngumu, hususan kwa wanawake, ambapo kwa Anastasia mkulima huyo kutoka Cameroon anasema anajihusisha na upandaji na hatua nyingine zote za kuzalisha mpunga kwa kutumia vifaa duni au kukosa kabisa, tofauti na wanaume wanaojihusisha na ukulima wa zao hilo katika kijiji hicho, ambao inakuwa rahisi kwao kupewa mikopo au kupata matrekta kurahisisha kazi yao.

Mkulima huyo ameliambia shirika la habari la IPS kuwa wanawake wana matatizo mengi, kwani hawana mamlaka ya kumiliki ardhi na kujikuta mara nyingi wakilima kwenye mashamba yanayomilikiwa na wanaume,na wanaelekezwa kulima maeneo yanayolimwa kwa kutumia matrekta na kwa sababu hiyo ni wazi kwamba wanaotumia matrekta watamaliza kwanza ndipo wanawake wafuate nyuma.

Teknolojia ni kikwazo kikubwa

Anasema kilimo cha mpunga kingekuwa rahisi kwake ikiwa angekuwa na teknolojia ya kumrahisishia kufanya kazi kama vile mashine ya kupukuchua mpunga, vifaa vya kupalilia magugu na vifaa vingine muhimu vinavyotumika katika kilimo cha mpunga, lakini kama ilivyo kwa wanawake wengi Afrika, hana uwezo wa kuvipata kirahisi.

Kutokana na matokeo ya utafiti uliofanywa na kituo cha utafiti wa zao la mpunga, kanda ya Afrika unaonyesha kuwa ikiliganishwa na wanawake, wanaume katika sekta ya kilimo wana nafasi kubwa ya kupata rasilimiali kama vile umiliki wa ardhi, kupata mitaji, elimu na vifaa vya kisasa vya kilimo, na hiyo inachangiwa na tamaduni zilizopo na uwezo kiuchumi.

Kwa mujibu wa mtaalamu wa masuala ya jinsia katika kituo hicho, Afiavi Aghbor-Noameshie, hakuna mfumo mzuri wa kijinsia katika sekta ya kilimo cha mpunga Afrika, kwani wanawake wanashiriki kikamlilifu katika shughuli zote za kilimo hicho kuanzia kwenye kupanda hadi kutafuta masoko, lakini hawapewi kipaumbele katika suala la teknolojia.

Kwa sasa, Afrika inaongoza kuagiza mchele kutoka nje kutokana na kutumia zaidi ya inachozalisha, ambapo mwaka jana bara hilo lilitumia jumla ya dola bilioni 5 za Marekani kuagiza tani 12 za mchele kutoka nje.

Kilimo cha jembe la mkono kinarudisha nyuma maendeleo ya wanawake.
Kilimo cha jembe la mkono kinarudisha nyuma maendeleo ya wanawake.Picha: CC-BY-SA-cimmyt

Mageuzi ya kweli yataletwa na wanawake

Na ili kuleta mageuzi ya kweli katika sekta hiyo, wanawake wametakiwa kushirikishwa ipasavyo katika maendeleo ya ukulima wa zao hilo.

Wataalamu wa masuala ya jinsia wamesema kuwa suala la jinsia ni lazima lijadiliwe kwa upana ili kuizingatiwa katika sekta ya kilimo,na hivyo kuwa na mgawanyo sawa wa kazi.

Kwa upande wake, mtaalamu wa masuala ya kilimo na jinsia katika kituo cha kimataifa cha uvumbuzi na mpangilio wa chakula cha chuo kikuu cha Michigan, Nathalie Me-Nsope amesema haiwezekani kuzungumzia maendeleo ya kilimo wakati ikifahamika wazi kuwa wanawake bado wana matatizo mengi yanayowakabili na hivyo kuwa kikwazo katika uzalishaji na upatikanaji wa soko la zao hilo.

Mwandishi: Flora Nzema/IPS

Mhariri: Saumu Yusuph Mwasimba