1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanawake bado wakabiliwa na unyayasaji usioripotiwa

25 Novemba 2019

Wakati ulimwengu ukiadhimisha Siku ya Kupambana na Unyanyasaji Dhidi ya Wanawake, Umoja wa Mataifa ametoa wito wa kuchukuliwa hatua kali zaidi za kuwalinda wanawake ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/3TewC
Belgien Demo Gegen Gewalt gegen Frauen in Brüssel
Picha: Reuters/F. Lenoir

Katibu Mkuu wa Umoja huo, Antonio Guterres, amenukuliwa akizitolea wito mamlaka na sekta binafsi na jamii kwa ujumla kuchukua hatua madhubuti kupinga unyanyasaji wa kingono dhidi ya wanawake pamoja na chuki dhidi yao.

Maadhimisho ya siku hii yanafanyika wakati bado wanawake wanakabiliwa na visa vya unyanyasaji wa kingono ambavyo kwa kiasi kikubwa haviripotiwi. Lakini pia wanawake na hata watoto hususan masikini na wanaotoka vijijini, kuuzwa mijini na watu wanaowaahidi kupata kazi nzuri, lakini badala yake hujikuta wakiwa katikati ya biashara ya utumwa mambo leo.

Kulingana na takwimu za hivi karibuni za uhalifu za India nchi hiyo ilirekodi visa 3,000 vya biashara haramu ya binaadamu mwaka 2017 takwimu ambazo zinakosolewa na wanaharakati.

Huko Ubelgiji, jana karibu wanawake 10,000 waliandamana kupinga unyanyasaji dhidi yao. Walifika hadi mbele ya jengo la mahakama wakiwa na viatu vyekundu kuashiria wanawake waliouawa nchini humo tangu mwaka 2017 ati kwa sababu tu wao ni wanawake.

Mratibu wa maandamano hayo Julie Wauters amesema, wanawake 99 walikuwa wahanga wa mauaji hayo yaliyojulikana kama "femicide" tangu mwaka 2017. Hata hivyo hakukua na idadi maalumu kutoka serikalini.

Wanawake wa Brussels waliweka viatu vyekundu mbele ya jengo la mahakama wakipinga mauaji ya wenzao.
Wanawake wa Brussels waliweka viatu vyekundu mbele ya jengo la mahakama wakipinga mauaji ya wenzao.Picha: AFP/K. Tribouillard

''Kilio cha waandamanaji ni cha kuungana na wanawake kote duniani. Unaweza kuwa umesikia wanawake na wanaume wakipaza sauti. Na ujumbe wao ni kuachwa kwa vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake na aina zote za uonevu." alisema Wauters.

Baadhi yao walijipaka rangi usoni kuashiria wanawake wanaopigwa ngumi na wanaume.

Mashambulizi dhidi ya wanawake hayaripotiwi

Nchini Mongolia, vitendo vingi vya unyanyasaji wa kingono dhidi bado haviripotiwi, kwa sababu hakuna sheria maalumu ya kuwalinda. Sheria kuhusu makosa kama hayo ilianzishwa mwaka 2015 lakini iliondolewa miaka miwili baadae baada ya wanasiasa kudai kwamba inaweza kutumika vibaya.

Sheria kuhusu usawa wa kijinsia inasema taasisi zote zinatakiwa kuwa na sera zao wenyewe za kupambana na unyanyasaji wa kingono, lakini hakutakuwa na hatua zozote iwapo hawatakuwa na sera za aina hiyo.

Belgien Demo Gegen Gewalt gegen Frauen in Brüssel
Miongoni mwa waandamanaji wanaopinga unyanyasaji dhidi ya wanawakePicha: AFP/K. Tribouillard

Utafiti uliofanywa na tume ya haki za binaadamu ya kitaifa nchini humo, NHRC mwaka 2017 umeonyesha asilimia 63 ya wanawake walinyanyaswa kingono na wakubwa wao wa kazi. Mwanamke mmoja alisema bado anajikongoja kurejea kwenye hali ya kawaida baada ya mwajiri wake kujaribu kumbaka miaka 12 iliyopita akiwa ofisini.

Unyanyasaji wa wanawake dhidi ya wanawake

Unyanyasaji kwa wanawake wanaojifungua pia ni tatizo kubwa ambalo haliripotiwi. Uchunguzi wa mwezi uliopita, umeonyesha asilimia 42 ya wanawake walikumbana na unyanyasaji wa maneno, vitendo ama ubaguzi wakati wa kujifungua kwenye vituo vya afya. Wengine walipigwa ngumi, makofi, kukaripiwa au hata kudhihakiwa.

Utafiti huo ulifanywa na shirika la Umoja wa Mataifa la afya, WHO kwa wanawake 2,016 waliokuwa katika uchungu wa kujifungua na 2,672 baada ya kujifungua.

Kulingana na uchunguzi huo zaidi ya theluthi moja ya wanawake nchini Ghana, Guinea, Nigeria na Myanmar walikumbwa na visa hivyo ingawa unahitimisha kwamba unyanyasaji kama huo pia unatokea kwenye mataifa yaliyoendelea.

Vitendo hivyo vya unyanyasaji viliongezeka dakika 30 kabla ya kujifungua hadi dakika 15 baada ya kujifungua. Asilimia 30 ya visa vya upasuaji na asilimia 75 ya wanawake wanaoongezewa njia vilifanywa bila ya mama kuarifiwa na mara nyingi bila ya sindano ya ganzi. Asilimia 57 ya wanawake waliohojiwa baada ya kujifungua wamesema hawakupewa dawa za kupunguza maumivu. 

Ukiachilia mbali hayo baadhi ya wanawake walizuiliwa kuondoka baada ya kujifungua kwa kuwa tu walikosa fedha za kulipia huduma za kujifungua.