Wanasiasa Haiti watafuta ushirikiano mpya wa kuongoza nchi
7 Machi 2024Wanasiasa wa Haiti wameanza kutafuta muungano mpya wa ushirikiano, unaoweza kuliondoa taifa hilo katika ghasia za magenge ya wahalifu ambayo yameiweka nchi hiyo katika hali ya sintofahamu.
Kiongozi wa zamani wa waasi Guy Philippe na mgombea wa zamani wa urais na seneta Moïse Jean Charles, wamesema kuwa wamesaini makubaliano ya kuunda muungano wa kuongoza nchi.
Philippe, ambaye ni kinara katika uasi wa 2004, uliomwondoa madarakani rais wa zamani Jean-Bertrand Aristide, alirejea nchini humo mwezi Novemba. Tangu wakati huo amekuwa akimshinikiza waziri mkuu Ariel Henry kujiuzulu.
Hadi sasa hali bado ni tete, huku shule, biashara na uwanja wa ndege vikisalia kufungwa. Waziri Mkuu Henry anayekabiliwa na shinikizo la kujiuzulu ameshindwa kurejea nchini humo na kukimbilia kisiwa cha Puerto Rico.