Wabunge Marekani wahoji usiri wa uwepo wa jeshi lao Afrika
4 Novemba 2017Kuuawa mwezi uliyopita kwa wanajeshi wanne wa Marekani katika shambulizi la kuvizia nchini Niger kumemulika suala hilo, ambapo wabunge sasa wanatoa wito wa kuwepo na uwazi zaidi juu ya kinachoendelea barani Afrika.
Seneta wa chama cha Democratic Tim Kaine, alisema wiki hii kuwa uwepo wa kijeshi wa Marekani barani Afrika ni mkubwa kuliko umma unavyojua.
Shambulio la Niger limeasha pia mjadala juu ya mamlaka ya kisheria inayoitumia wizara ya ulinzi kupambana dhidi ya makundi ya itikadi kali nje ya taifa hilo, hususani barani Afrika ambako wanajeshi karibu 6,000 wamewekwa. Waziri wa ulinzi Jim Mattis alikumbana na maswali ya wabunge wiki hii kuhusu sheria hizo za kupigana vita.
Mattis, Tillerson: Sheria bado zinahitajika
Sheria hizo zilipitishwa awali siku tatu baada ya shambulizi la Septemba11, 2001 mjini New York na Washington, kwa lengo la kupambana na kundi la Al-Qaeda lakini tangu wakati huozimekuwa zikitumiwa kuwasaka wapiganaji wa Kiislamu kutoka makundi mengine tofauti.
Wabunge wa Marekani wanazingatia kuzirekebisha sheria hizo au kuzifuta, lakini Mattis na waziri wa mambo ya nje Rex Tillerson hawadhani iwapo zinapaswa kubadilishwa au kufutwa bila kuwepo na sheria mbadala.
Mattis alisema kundi la Al-Qaeda hivi sasa limegawika katika makundu mengine, likiwemo kundi la Dola la Kiislamu, na kwa sababu hiyo sheria hizo bado zinatumika. Aliwambia wabunge kuwa makundi hayo yanatengana, na kisha kurudi pamoja, yanaweza kubadili majina yao mara kadhaa kama zifanyavyo bendi za muziki.
Seneta wa Democratic Chris Coons, alisema janga lililotokea nchini Niger, la kupotolewa na wanajeshi wao wanne, lilisaidia kuwavutia nadhari juu ya ukweli kwamba wanao raia, na wanao maseneta wasio wakweli kuhusu hasa wapi duniani wanashiriki dhidi ya adui huyo anaebadilika katika zama mpya za mapigano.
Askari 6,000 katika mataifa 11
Marekani wiki hii iliahidi kiasi cha dola milioni 60 kusaidia kikosi cha kupambana na ugaidi katika kanda ya Sahel maarufu G5. Wanachama wa G5, Burkina Faso, Chad, Mali, Mauritania na Niger, wanaangaliwa na Marekani kama washirika wa kikanda.
Rasmi, ujumbe wa Marekani katika eneo la Afrika una jukumu la kutoa mafunzo, ushauri na msaada kwa majeshi ya Kiafrika ili kusaidia mataifa kusimama dhidi ya makundi ya itikadi kali. Lakini kiuhalisia, kama ilivyoonyeshwa nchini Niger, jukumu la Marekani linakwenda mbali ya hilo.
Kulingana na taarifa kutoka Ikulu ya Marekani kwenda Congress mwezi Juni, wanajeshi walio tayari kwa mapambano wameplekwa katika mataifa 19 -- na 11 kati yake ni katika bara la Afrika - ambayo ni Somalia, Libya, Kenya, Niger, Cameroon, Uganda, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Djibouti na Misri.
Kufichuka kwa mauaji ya wanajeshi
Kwa seneta Mrepublican Rand Pual, ujumbe rasmi wa mafunzo ni kisingizio tu cha kuficha ukweli hasa kile kinachoendelea. Inaonekama kama vile una mgogoro unaoendelea nchini Niger. Tuna wanajeshi 6,000 katika mataifa 54 barani Afrika," Paul alimuambia Mattis.
Kulingana na Pentagon, tukio la Niger lilitokea mapema mwezi Oktoba, wakati timu ya Marekani na Niger ikifanya doria ya kawaida katika kijiji cha Tongo Tongo karibu na mpaka wa Mali. Walishambuliwa na wapiganaji karibu 50 wa ndani wanaohusishwa na kundi la Dola la Kiislamu.
Kituo cha ABC News kiliripoti siku ya Alamisi kuwa ujumbe huoulibadilika na kimsingi walikuwa wakijaribu kumteka au kumuua kiongozi wa wapiganaji mwenye mafungamano na Dola la Kiislamu na Al-Qaeda.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef