1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasayansi waonya kuhusu Ebola

22 Oktoba 2014

Wanasayansi wamesema kwamba kuwapima wasafiri katika maeneo yaliyoathirika na ugonjwa hatari wa Ebola kabla hawajasafiri kuelekea maeneo mengine, ni hatua muhimu katika kuepusha kuenea kwa ugonjwa huo.

https://p.dw.com/p/1Da1S
Ebola Screening Heathrow London Großbritannien 14.10.
Uchunguzi wa Ebola katika uwanja wa ndege wa LondonPicha: picture-alliance/dpa

Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti iliyochapishwa Jumanne wiki hii na jarida la sayansi la Lancet, watu watatu wenye virusi vya Ebola wanaweza kusafiri katika nchi ya kigeni kila mwezi kutokea nchi tatu za Afrika Magharibi zilizokabiliwa na mlipuko wa Ebola. Nyamiti Kayora na maelezo zaidi.

Mataifa hayo matatu, Guinea, Liberia na Sierra Leone, yanafanya vipimo kwa wasafiri kubaini kama wana homa, ingawa uchunguzi huo hauwezi kubainisha mgonjwa wa Ebola papo kwa hapo kabla hajaonesha dalili katika kipindi kinachoweza kufikia siku 21.

Ripoti ya utafiti iliyochapichwa katika jarida la matibabu la Lancet limesema uchunguzi wa wasafiri wanaotoka nje unaweza kuwa moja ya njia za kupunguza kuenea kwa Ebola.

Ebola Grenzkontrolle in Liberia
Kituo cha kuchunguza Ebola nchini LiberiaPicha: AFP/Getty Images/Z. Dosso

Kwa kutumia mfumo wa safari za ndege za kimataifa zinazofanywa kwa mwaka huu 2014 na idadi ya wasafiri kwa mwaka 2013 pamoja na hali ilivyo sasa ya ugonjwa wa mripuko na kizuizi cha safari za ndege, utafiti unaonyesha kuwa wastani wa abiria watatu wameambukizwa ugonjwa wa ebola wanakadiriwa kusafiri kwa kutumia ndege za kimataifa kila mwezi.

Dr.Kamran Khan wa hospitali ya Michael iliyopo Toronto, Canada ambaye ameongoza utafiti huo anasema, utafiti unaonyesha kuwa inafaa zaidi na haileti usumbufu kwa wasafiri kuwachunguza abiria kutoka nchi zilizoathiriwa za afrika ya Magharibi wanapotaka kuondoka eneo hilo, kuliko kuwachunguzwa wakati wanapowasili nchi wanakokwenda, kama vile Marekani, Uingereza, Ufaransa na nchi zingine zilivyoanza kufanya.

Khan aliongeza kuwa wakati kuwachunguza abiria waliowasili katika viwanja vya ndege wakitokea nje za nchi za Afrika Magharibi kunaweza kuimarisha hisia za usalama, na hii inaweza pengine kuleta mafanikio mazuri lakini kidogo, na inaweza kuondosha rasilimali muhimu kutoka kwa jitihada za kuimarisha huduza za afya ya umma,ambazo zina manufaa makubwa zaidi.

Ebola Gefahr USA
Hofu ya ugonjwa wa Ebola yatanda nchini MarekaniPicha: Reuters/Jaime R. Carrero

Ebola imewaua watu zaidi ya 4,500 nchini Liberia, Sierra Leone na Guinea. Lakini huku angalu nusu ya visa vya maambukizi vikiw ahaviripotiwi kabisa na kasi ya vifo kutokana na Ebola ikifikia asilimia 70 kwa mujibu wa makadirio ya shirika la afya duniani, WHO, idadi halisi ya vifo kutokana na mlipuko wa sasa wa Ebola unaelezwa kuwa mbaya kabisa katika historia pengine ni zaidi ya 12,000.

Visa vya homa ya kuvunja damu vimshawahi kusambaa hadi nchini Nigeria, Senegal, Uhispania na Marekani na shirika la afya duniani limesema haiwezi kuzuilika kuwa visa vya Ebola vitaripotiwa katka nchi nyingi zaidi.

Wataalamu wengi wa matibabu wamehoji kwamba mahala pazuri pa kuzuia kuenea kwa Ebola ni katika chanzo chake.

Khan alisema vikwazo vingi vya usafiri wa anga vinaweza kuwa na
madhara makubwa ya kiuchumi ambayo yanaweza kudhoofisha kanda ya Afrika Magharibi na pengine kuvuruga usafirishaji wa vifaa muhimu ya afya na utoaji wa
huduma za kibinadamu.

Utafiti umebaini kuwa takriban wasafiri 500,00 waliosafiri katika safari za kibiashara mwaka 2013 kutoka nje Conakry, Monrovia na Freetown, zaidi ya nusu walikuwa wakielekea moja kati ya nchi tano, zikiwemo Ghana, Senegal, Uingereza, Ufaransa na Gambia.

Ripoti hiyo pia imebaini kuwa zaidi ya asilimia 60 ya wasafiri mwaka 2014 kwa kiwango kikubwa walikuwa wakielekea mataifa masikini au yenye kipato cha wastani,ambako raslimali za dawa na afya ya umma kuzuia mlipuko mkubwa kwa kwiango kikubwa huenda ni duni.

Mwandishi:Nyamiti Kayora/RTRE

Mhariri:Josephat Charo