1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanariadha walalamika Kenya kuhusu uteuzi wa kikosi cha Olimpiki London

2 Machi 2012

Wanariadha wa zamani wameishtumu mipango ya Kenya kukiteua sehemu ya kikosi kitakachoiwakilisha nchi hiyo katika mashindano ya mwaka huu ya Olimpiki, kwa kuzingatia mbio zitakazoandaliwa Marekani.

https://p.dw.com/p/14DNp
Wanariadha wakizitimka mbio za mita 1,500 mjini Daegu, Koera Kusini
Wanariadha wakizitimka mbio za mita 1,500 mjini Daegu, Koera KusiniPicha: dapd

Wanariadha hao wa zamani wanahoji kuwa hakukuwa na haja ya kukiuka desturi ya kutumia mfumo wa majaribio ya kitaifa katika vitengo vyote vya mbio, ili kuwateuwa watakaofuzu.

Wiki iliyopita mwenyekiti wa chama cha riadha nchini Kenya Athletics Kenya Isaiah Kiplagat alisema kuwa wanariadha watano wa kiume na kike watashiriki katika mbio za mita 5,000 na 10,000 katika mashindano ya Diamond League, mjini Eugene, Oregon mapema mwezi Juni. Kisha wale watakaochukua nafasi tatu za kwanza watajiunga na kikosi cha Olimpiki.

Kiplagat alisema aliwataka wanariadha hao wachaguliwe katika mbio za mwinuko wa chini kabla ya kuendelea na mazoezi yao katika muinuko wa juu tayari kwa mashindano ya Olimpiki ya London.

Wale watakaosalia watachaguliwa kupitia zoezi la majaribio mjini Nairobi mwezi Juni. Lakini bingwa mara tano wa ulimwengu wa mbio za nyika na mshikilizi wa zamani wa rekodi ya ulimwengu ya Marathon Paul Tergat amesema majaribio hayo yanafaa kuandaliwa nchini Kenya jinsi ilivyokuwa desturi. Alisema haelewi ni kwa nini kikosi cha Kenya kichaguliwe nchini Marekani.

Nembo ya mashindano ya Olimpiki jijini London mwaka huu
Nembo ya mashindano ya Olimpiki jijini London mwaka huuPicha: picture-alliance/dpa

Naye mwanariadha Martin Keino alisema mbio za majaribio zinazoandaliwa Kenya huwapa maelfu ya mashabiki fursa ya kuwaona nyota wao kabla ya kwenda katika olimipiki, akiongeza kuwa mazoezi ya muinuko wa juu nchini Kenya yatawanufaisha wanariadha kuliko yale ya muinuko wa chini kule Oregon Marekani.

Mkondo wa pili wa kombe la Ligi ya Mabingwa Afrika

Katika soka Mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Zamalek na Yanga itachezwa Jumamosi hii tarehe 3 Machi kwenye Uwanja wa Jeshi jijini Cairo Misri kuanzia saa 12 jioni kwa saa za Misri. Shirikisho la Kandanda Afrika (CAF) limesema mechi hiyo itachezwa katika uwanja mtupu kwa vile Zamalek inakabiliwa na adhabu ya kucheza mechi hiyo bila mashabiki. Shirikisho la Soka Tanzania TFF limesema msafara wa Yanga utakuwa na watu 40 pekee watakaokuwa uwanjani Misri kwa mchuano huo.

Adhabu ya Zamalek kutocheza mechi mbili za nyumbani za michuano hiyo bila mashabiki ilitolewa Aprili 20 mwaka jana na Bodi ya Nidhamu ya CAF iliyokutana jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Mechi dhidi ya Yanga ndiyo itakayokuwa ya kwanza kwa Zamalek kuanza kutumikia adhabu hiyo iliyotokana na mashabiki wake kufanya fujo kwenye mechi ya michuano hiyo mwaka jana ilipocheza dhidi ya Club Africain ya Tunisia.

Zamalek kucheza ndani ya uwanja mtupu Cairo
Zamalek kucheza ndani ya uwanja mtupu CairoPicha: picture alliance / dpa

Wakati huo huo, mabingwa wa ligi ya taifa nchini Kenya, Tusker FC wako mjini Kigali, Rwanda ambako watachuana na APR katika pambano la marudiano la Kombe la Mabingwa Afrika: Tusker walitoka sare ya bila kufungana na APR mjini Nairobi wiki mbili zilizopita. Kocha wa Tusker Sammy Omollo anasema wanataraji angalau kutoka sare ya kufungana ndiposa wawe na nafasi ya kuendelea. Mechi hiyo itachezwa Jumapili saa kumi jioni. Uganda Revenue Authority itakuwa ugenini kupambana na Lesotho Correctional Services. Katika mchuano wa kwanza URA iliizaba LCS magoli matatu kwa nunge. Klabu ya Mafunzo ya Zanzibar itafunga kazi ugenini dhidi ya Liga Muculmana ya Msumbuji. Vijana hao wa Zanzibar walifungwa magoli mawili kwa nunge katika mechi ya kwanza.

Katika mechi za marudiano za Kombe la Shirikisho, klabu ya Simba ya Tanzania itawakaribisha Kiyovu Sport ya Rwanda. Mechi hiyo itachezwa Jumapili hii tarehe 4 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa mjini Kigali, timu hizo mbili zilitoka sare ya kufungana bao moja. Gor Mahia ya Kenya ambayo ililazwa na Ferroviario de Maputo ya Msumbiji magoli matatu bila jawabu kule mjini Maputo itacheza mechi ya marudiano mjini Nairobi Jumamosi ijayo tarehe kumi. Klabu ya Jamhuri kutoka Zanzibar itasafiri hadi Zimbabwe kuchuana na Hwange. Jamhuri walikuwa magoli matatu kwa nunge katika mchuano wao wa kwanza nyumbani Zanzibar.

Bayern kupigwa jeki na kurejea kwa Schweinsteiger

Katika klabu ya ligi ya Ujerumani – Bundesliga, Bayern Munich imesema mchezaji wake Bastian Schweinsteiger amerejelea mazoezi mepesi huku kiungo huyo wa kati akiendelea kupata nafuu kutokana na jeraha lake la kifundo cha mguu. Schweinsteiger alifanya mazoezi mepesi Alhamisi, wiki tatu baada ya kupata jeraha la kifundo cha mguu kwenye mchuano walioishinda Stuttgart magoli mawili kwa nunge. Kiungo huyo wa kati alikuwa tayari amekosa miezi miwili ya msimu kutokana na jeraha la mfupa wa shingo. Bayern imesema mazoezi yake yataimarika katika siku zijazo.

Kiungo wa Bayern Bastian Schweinsteiger
Kiungo wa Bayern Bastian SchweinsteigerPicha: dapd

Na klabu ya Schalke 04 imempa fursa nahodha wa zamani wa Real Madrid Raul Gonzalez kurefusha mkataba wake katika klabu hiyo ya Bundesliga. Meneja Mkuu wa Schalke Horst Heldt ayasema hayo wakati mkataba wa Raul ukitarajiwa kukalimika mwishoni mwa msimu huu. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 34 ameifungia Schalke magoli 25 kati ya mechi 56 za ligi tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2010 akitokea Real Madrid. Ameifungia klabu hiyo ya Ujerumani magoli 33 katika vinyang'anyiro vyote, yakiwemo magoli 14 msimu huu.

UN: Wanawake wakubaliwe kufunga hijab

Umoja wa Mataifa umelitaka Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA kuubatilisha uamuzi wake wa kupiga marufuku wanawake kuvalia hijab, ambacho ni kitambaa kinachovaliwa kichwani kwa Waislamu, wakati kitengo chake cha sheria kitakapokutana Jumamosi. Issa Hayatou, Rais wa Shirikisho la Soka Afrika CAF, na Zhang Jilong wa China, ambaye ni Kaimu Mkuu wa Shirikisho la Soka barani Asia AFC, pia wametangaza uungaji mkono wao kuhusu suala hilo pamoja na wachezaji kadhaa wa ligi ya Soka nchini Uingereza. Mwanamfalme Ali wa Jordan ambaye ni mwanachama mwenye umri mdogo zaidi katika kamati kuu ya shirikisho la FIFA atahutubia mkutano wa Bodi ya Kimataifa ya chama cha soka IFAB, Jumamosi mjini Bagshot, Surrey. Mwanamflame Ali alisema atasikitika sana ikiwa IFAB haitabadilisha uamuzi wake iliyoufanya Machi 2007 wa kuwapiga marufuku wanawake kuvaa hijab.

Timu ya soka ya wanawake ya Iran, ilizuiwa na refa kufuzu katika mashindano ya olimpiki London kwa sababu ya hijab.
Timu ya soka ya wanawake ya Iran, ilizuiwa na refa kufuzu katika mashindano ya olimpiki London kwa sababu ya hijab.Picha: picture-alliance/abaca

Wladmir kuchapana na Jean-Marc

Na Katika ndondi bingwa wa Ulimwengu Wladmir Klitschko huenda akakumbwa na uhaba wa wapinzani wakuu wa uzani wa juu, lakini anapanga kudhihirisha umahiri wake kwa kumwangusha Mfaransa Jean-Marc Mormeck Jumamosi. Bingwa huyo wa Ulimwengu Klitschko atatetea mataji yake ya IBF IBO WBO na WBA dhidi ya Mormeck ambaye alipanda ngazi kutoka kitengo cha Cruiserweight miaka miwili iliyopita. Pambanao hilo litaandaliwa mjini Dusseldorf Ujerumani. Mabondia hao walitarajiwa kuingia ulingoni mwezi Desemba lakini matatizo ya figo yalimkumba Klitschko na ikabidi pigano hilo liahirishwe. Litakuwa ni pigano la 60 la taaluma yake Kiltschko, na atalenga kulifanya kuwa la 50 kupitia njia ya knock out.

Mwanabondia wa uzani wa juu Wladmir Klitschko
Bondia wa uzani wa juu Wladmir KlitschkoPicha: picture alliance/dpa

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AFP

Mhariri: Josephat Charo