Wanaowania faida za kiuchumi wanazidisha mzozo wa Yemen-UN
27 Januari 2021Ripoti hiyo ya wataalamu ambayo nakala yake ilionwa na shirika la habari la Associated Press jana Jumanne, inawatuhumu waasi wa Kihuthi kuchukua kiasi cha dola bilioni 1.8 zilizokuwa zimetolewa mwaka 2019 kwa ajili ya kugharimia mahitaji ya msingi ya wananchi na mishahara kwa wafanyakazi wa serikali, na kuzibadilishia matumizi.
Soma zaidi: Marekani yasimamisha vikwazo dhidi ya waasi wa Yemen kuimarisha msaada
Kwa upande wa serikali, ripoti hiyo imesema dola milioni 423 zilizotolewa na Saudi Arabia kwa madhumuni ya kununua chakula na bidhaa nyingine za lazima kwa Wayemen wenye mahitaji, zilitumiwa kwa njia zisizo halali.
Wataalamu hao katika ripoti yao wamesema serikali ya Yemen na waasi wa Kihuthi wanaonekana kutojali athari za kuporomoka kwa uchumi wa taifa lao na dhiki inayowakabili raia wao, huku wakiendelea kufuja raslimali za kifedha na kiuchumi.
Matatizo mengi yanaweza kuepukika
Vita vya Yemen vinavyoendelea kwa miaka sita sasa vimeuwa watu wasiopungua 112,000, na kuifanya nchi hiyo kutumbukia katika mzozo mkubwa kabisa duniani kwa wakati huu, ulioharibu miundombinu na kuwaacha watu wake wakiwa na ukosefu mkubwa wa chakula.
Soma zaidi: Sera ya Marekani kuhusu Mashariki ya Kati itabadilishwa?
Akizungumzia madhila hayo, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema watoto wa Yemen wanaangamia kwa matatizo ambayo yangeweza kuepukika.
''Kwa wastani, kila dakika kumi, mtoto wa chini ya miaka mitano anakufa nchini Yemen kutokana na sababu zinazoepukika,'' amesema Guterres na kuongeza kuwa wengi wa watoto wanaonusurika huathiriwa na afya udumavu na afya duni maisha yao yote.
Washirika wagawika kimaslahi
Mgogoro ulianza mwaka 2014 baada ya uwaasi wa Kihuthi wanaoungwa mkono na Iran kuyakamata maeneo ya kaskazini wanakoishi watu wengi, hatua iliyofuatiwa na kampeni kubwa ya mashambulizi ya anga, yaliyofanywa na muungano wa nchi za kiarabu unaoongozwa na Saudi Arabia na kuungwa mkono na Marekani, kwa lengo la kuibakisha madarakani serikali ya mjini Sana'a.
Soma zaidi: 20 wauawa katika shambulio dhidi ya uwanja wa ndege Aden
Ripoti ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa imesema kuna ushahidi unaoongezeka kuwa watu binafsi au taasisi za nchi Iran huwapa Wahuthi silaha na zana nyingine za kivita. Imesema serikali ya Yemen ilipoteza maeneo makubwa kwa Wahuthi na kundi jingine linaloitwa Baraza la Mpito la Kusini, ambalo linaungwa mkono na Umoja wa Falme za Kiarabu.
Ingawa kundi hilo lilisaini makubaliano ya kugawana madaraka na serikali mwezi Desemba, ripoti hiyo imesema ugomvi wa ndani, na tofauti za kimaslahi katika nchi zinazowaunga mkono, vimekwamisha juhudi zao za pamoja dhidi ya Wahuthi.
Vyanzo: ape, rtre