Wanaotaka kujitenga wajaribu tena kumrejesha Puigdemont
6 Mei 2018"Hatutaki uchaguzi mpya," amesema Eduard Puyol, msemaji wa kundi linalomuunga mkono Pigdemont la Together for Catalonia, pamoja kwa Catalonia.
Hata hivyo juhudi kama hizo zitafanywa kumrejesha madarakani rais wa zamani wa Catalonia ifikapo Mei 14 aliongeza Puyol baada ya mazungumzo na Puigdemont mjini Berlin.
Puigdemont aliondolewa madarakani na serikali kuu mjini Madrid baada ya Catalonia kutoa tamko linalotangaza uhuru wa jimbo hilo mwaka jana kufuatia kura ya maoni iliyofanyika katika jimbo hilo ambayo haikuidhinishwa na serikali ya Uhispania.
Kiongozi huyo wa uhuru wa jimbo la Catalonia baadaye aliondoka na kwenda uhamishoni nchini Ubelgiji. Juhudi za hapo kabla za kutaka kumrejesha madarakani zilizuiliwa na mahakama ya Uhispania.
Puigdemont alikamatwa nchini Ujerumani Machi mwaka huu baada ya Uhispania kutoa waranti wa kukamatwa kwake barani Ulaya. Baadaye aliachiliwa kwa dhamana.
Siku ya Ijumaa bunge la Catalonia linalounga mkono uhuru wa jimbo hilo liliunga mkono sheria inayoruhusu kurejeshwa kwake madarakani wakati akiwa nje ya nchi, kitu ambacho serikali ya Uhispania imekataa.
Rais Halali
Ines Arrimadas, kiongozi jimboni Catalonia wa chama kinachopinga uhuru Ciudadamos Party, ameikataa sheria hiyo aliyoiita ya "Puigdemont", akiieleza kuwa "imetengenezwa kwa ajili ya mkimbizi".
Tangu alipoikimbia Uhispania Puigdemont amekuwa mtu anayesababisha mgawanyiko miongoni mwa wanaotaka kujitenga.
Siku ya Jumamosi kundi lenye ushawishi mashinani linalounga mkono uhuru la ANC lilitangaza matokeo ya uchunguzi wa maoni, likisema kwamba wengi wa wanachama wake wanaunga mkono kurejea kwa "rais halali".
Hata hivyo , iwapo hilo litashindikana, waungaji mkono wa ANC wanataka serikali mpya iundwe bila ya kurejea katika upingaji kura.
Bunge la jimbo hilo linapaswa kuchagua rais mpya ifikapo Mei 22 ama itayarishe uchaguzi mpya.
Iwapo Puigdemont hatarejeshwa madarakani, waungaji wake mkono watapendekeza kwamba kiongozi wa ANC Jordi Sanchez, ambaye kwa sasa yuko kifungoni mjini Madrid kuhusiana na juhudi za kudai uhuru kushindwa, apewe kazi hiyo.
Lakini mwezi uliopita mahakama kuu ya Uhispania ilikataa ombi la Sanchez kutolewa kutoka jela na kuapishwa kama kiongozi wa jimbo hilo.
Iwapo hatua hiyo itashindikana "tutafungua mlango wa uwezekano mwingine," Pujol aliwaambia waandishi habari mjini Berlin, na kuongeza kwamba "hakuna jina mlilotabiri ambalo linajadiliwa". Vyombo vya habari vya Uhispania vilitaja jina la mtaalamu wa uchumi Elsa Artadi, ambaye ni mshirika wa Puigdemont.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Caro Robi