Wananchi wa Rwanda wapiga kura
4 Agosti 2017Maafisa wachache wa usalama walionekana mjini Kigali wakati wapiga kura wakipanga mistari mirefu katika vituo vya kupigia kura kushiriki uchaguzi wa urais, saa chache kabla ya vituo hivyo kufunguliwa mapema saa moja asubuhi. Takriban watu milioni saba wamesajiliwa kupiga kura nchini humo.
Paul Kagame, aliye na miaka 59, anakabiliwa na wapinzani wawili tu, Frank Habineza kutoka chama kidogo cha Democratic Green Party – ambacho ni chama pekee cha upinzani kilichosajiliwa. Mwengine ni mgombea wa kujitegemea, mwandishi habari wa zamani, Philippe Mpayimana.
"Hata kama mimi ni masikini nimempigia kura Rais Kagame kwa kurejesha amani ya nchi," alisema mkulima mmoja aliye na miaka 45, Appolinaire Karangwa, mara baada ya kupiga kura yake mjini Kigali.
Itakumbukwa kuwa katika kura ya maoni ya mwaka 2015, Rais Kagame aliungwa mkono kwa asilimia 98 ya kura zilizopigwa kumruhusu kubadilisha katiba ili kusalia madarakani kwa mihula mitatu, ambapo huenda akabakia madarakani hadi mwaka 2034. Rais huyo wa Rwanda alichaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka wa 2000.
Kagame adaiwa kuukandamiza upinzani
Chama chake cha RPF kimesalia madarakani tangu kiliposhinda utawala wa kiraia na kijeshi nchini humo mwaka wa 1994 na kumaliza mauaji ya kimbari yaliyosababisha mauaji ya watu 800,000 kutoka makabila ya Kitutsi na Kihutu.
Kwa upande mwengine, wakosoaji wa rais huyo wanadai kwamba Kagame amekuwa akiukandamiza upinzani kwa mauaji huku makundi ya kutetea haki za binaadamu yakidai Paul Kagame anakiuka haki za binaadamu pamoja na kuvinyamazisha vyombo vya habari.
Lakini mbali ya hayo, Rais Kagame amekuwa akimiminiwa sifa kwa kuibadilisha nchi hiyo iliyokumbwa na mauaji ya kimbari na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kuwa moja ya nchi imara barani Afrika.
Katika utawala wake kumekuwepo na ukuaji mkubwa kiuchumi wa asilimia 8 kati ya mwaka 2001 na 2015 na hata kuibadilisha Rwanda kuwa kitongoji cha teknolojia huku akikomesha ufisadi.
Jumuiya ya Kiuchumi ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, COMESA, na Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC, wametuma waangalizi wao katika uchaguzi huu ambapo matokeo rasmi yanatarjiwa kutolewa ndani ya wiki moja.
Upigaji kura utamalizika hii leo mwendo wa saa tisa mchana huku matokeo ya kwanza yakitarajiwa kutolewa baadaye leo jioni.
Mwandishi: Amina Abubakar/dpa/Reuters/AP
Mhariri: Mohammed Khelef