1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wananchi wa Botswana wapiga kura leo

Kabogo Grace Patricia16 Oktoba 2009

Uchaguzi huo unaelekea kukichagua tena chama tawala cha Botswana Democratic

https://p.dw.com/p/K7pY
Kagiso Nazrullah Ntime, kiongozi wa tawi la vijana la chama cha upinzani cha Botswana National Front.Picha: Katrin Gänsler

Wananchi wa Botswana leo wanapiga kura kuchagua wabunge wa nchi hiyo, huku chama tawala cha rais wa sasa Ian Khama, kikitarajiwa kurejeshwa tena madarakani katika taifa hilo tajiri kwa kutengeneza almasi na taifa linaloonekana kuwa na demokrasia.

Uchaguzi huo ni changamoto kubwa kwa chama tawala cha Rais Khama cha Botswana Democratic Party, ambacho kiko madarakani tangu nchi hiyo ipate uhuru wake mwaka 1966 na ambacho kinakabiliwa na mivutano. Huku baadhi ya wakosoaji wa ndani wakikosoa aina yake ya kutawala, rais huyo ni al-maarufu sana nchi za nje, hasa kwa kupingana na viongozi wenzake na kumshutumu Rais Robert Mugabe wa nchi jirani ya Zimbabwe.

Maoni ya waangalizi wa Uchaguzi

Fransisco Madeira, Mkuu wa waangalizi wa uchaguzi huo kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), amesema hadi sasa hawajapokea malalamiko yoyote kutoka vyama vya siasa. Katika eneo la kaskazini-magharibi mwa Gabarone, Malebogo Morakaladi, mwenye umri wa miaka 36, amesimama kwenye mstari huku akisoma kitabu akisubiri zamu yake ifike ili apige kura. Anasema ni njia nzuri kupoteza muda kwa kusoma kitabu akiongeza kuwa uchaguzi kimekuwa kitu cha kusisimua katika miaka ya hivi karibuni.

Idadi ya waliojiandikisha

Kiasi watu 725 wameandikishwa kupiga kura katika vituo 2,288 vya kupigia kura nchini kote. vyama saba vya siasa na wagombea binafsi 15 wanagombea kinyang'anyiro katika majimbo 57, ikiwa ni viti vya bunge 57 na wabunge wa ziada wanne ambao wanachaguliwa na rais. Ili kushinda katika uchaguzi huo, chama kinahitaji kupata viti 29 ili kumtangaza rais wao. Matokeo ya uchaguzi huo yanatarajiwa kutangazwa kesho Jumamosi.

Otsweletse Moupo, wa chama kikuu cha upinzani cha Botswana National Front ana matumaini ya kutumia hali ya kutoridhika pamoja na mvutano wa ndani katika chama tawala na matatizo ya kiuchumi katika jamii.

Rais Ian Khama, mwenye umri wa miaka 56, ambaye ni mtoto wa rais wa kwanza wa nchi hiyo, Seretse Khama, huu utakuwa uchaguzi wake wa kwanza tangu alipochukua madaraka kutoka kwa mtangulizi wake Festus Mogae mwezi Aprili. Akizungumza jana Alhamisi katika mkutano, Rais Khama alisema hatosita kuwafukuza kazi viongozi wazembe kwa sababu hawana nafasi katika serikali yake.

Idadi ya wananchi wa Botswana

Botswana yenye idadi ya watu milioni 1.9, imeaajiri zaidi ya watu 5,000 katika sekta ya madini ya almasi, sekta inayochangia theluthi ya pato jumla la taifa. Nchi hiyo pia inakabiliwa na wagonjwa wa Ukimwi ambapo katika kila watu wazima wanne, mmoja kati yao ameambukizwa virusi vya HIV na asilimia 47 ya watu wanaishi chini ya kiwango cha umasikini cha dola moja kwa siku.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri: Othman Miraji