Wananchi Venezuela waunga mkono mabadiliko ya katiba
16 Februari 2009Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi ya Venezuela, Katika kura hiyo iliyofanyika jana Rais Chavez amepata asilimia 54 ya kura na kumfanya kuendelea kuwania urais hata baada ya kumalizika kwa kipindi chake cha miaka kumi mwaka 2013.
Akihutubia maelfu ya wafuasi wake muda mfupi uliyopita mara baada ya matokeo hayo kutangazwa, Rais Chavez amesema kuwa matokeo hayo yamepanua wigo wa majaaliwa ya nchi hiyo.
Rais Chavez ambaye ni mfuasi mkubwa wa siasa za kiongozi wa zamani wa Cuba Fidel Castro, amesema kuwa Venezuela kamwe sasa haitorudi katika zama za zamani alizoziita za kudhalilishwa na kudharauliwa.
Ushindi huo ni pigo kubwa kwa upinzani uliyosambaratika ambao katika miaka ya hivi karibuni uliweza kupiga hatua kuvuta uungwaji mkono.
Chavez aliingia madarakani mwaka 1999 kwa ahadi ya kupambana na rushwa ambapo amekuwa akiungwa mkono na watu wa hali ya chini kutokana na kuboresha sekta ya huduma za afya, shule pamoja na misaada ya chakula.