Wanamgambo wateka bwawa Iraq
7 Agosti 2014Baada ya wiki kadhaa za kujaribu wapiganaji wa kundi hilo walifanikiwa kulivamia bwawa hilo la Mosul na kuvilazimisha vikosi vya Wakurdi kuondoka kutoka eneo hilo.Hayo ni kwa mujibu wa waakazi wanaoishi karibu na bwawa hilo waliozungumza na shirika la habari la AP kwa sharti la kutotajwa majina kutokana na kuhofia usalama wao.
Kundi la Dola la Kiislamu limeweka taarifa kwenye mtandao leo hii ikithibitisha kulidhibiti bwaha hilo na kuapa kuendelea kusonga mbele katika vita vyao hivyo na kuongeza kusema kwamba hawatoachana na nia yao ya kuanzisha utawala mkubwa wa Kiislamu wa Khalifa.
Taarifa hiyo haikuweza kuyakinishwa lakini imewekwa wovuti unaotumiwa sana na kundi hilo.
Wakurdi waregeza msimamo
Maafisa kutoka eneo la mamlaka ya ndani la Wakurdi ambalo ndio lenye vikosi pekee vinavyopambana na kusonga mbele kwa wapiganaji hao wa itikadi kali kaskazini mwa nchi hiyo hawakuweza kupatikana kuzungumzia tukio hilo.
Kikosi cha Wakurdi cha Peshmerga huko nyuma kiliweza kuzuwiya kusonga mbele kwa wanamgambo wa Dola la Kiislamu lakini harakati zao zimeanza kupunguwa nguvu katika wiki za hivi karibuni.
Bomu laripuka Baghdad
Habari za kutekwa kwa bwawa hilo la Mosul au Bwawa la Saddam kama lilivyokuwa likijulikana hapo zamani zinakuja wakati mashambuliaji wa kujitowa muhanga maisha akiwa amejiripua leo hii katika kituo cha ukaguzi wa polisi mjini Baghdad na kuuwa takriban watu katika mtaa ulitokea mripuko huo wa al-Jiddah."
Watu zaidi ya 40 wamejeruhiwa katika mripuko huo uliotokea katika kitongoji kinachokaliwa na Washia wengi kusini mashariki ya Baghdad.
Hapo jana usiku mfululizo wa mirupuko ya mabomu umeuwa watu 51 mjini Baghdad.
Mwandishi :Mohamed Dahman/AP
Mhariri :Yusuf Saumu