Wanamgambo wa Taliban wajiimarisha Afghanistan
14 Agosti 2018Kwa mujibu wa Mohammad Tahir Rahmani kiongozi wa ngazi ya juu wa jimbo la Faryadb wanamgambo wa Taliban wamekamata vifaru na silaha kadhaa katika kambi ya jeshi ya Chenayeeha iliyoko jimbo la Faryab tangu mapigano yalipoanza tena Jumapili iliyopita.
Anasema hadi sasa vikosi vya serikali havijafanikiwa kuingia katika kambi hiyo ya jeshi na kuwa sehemu kubwa bado iko chini ya udhibiti wa wanamgambo wa Taliban.
Rahman ametaja idadi ya watu waliouawa lakini afisa mmoja wa jimbo nchini humo aliongeza kuwa wanamgambo wa Taliban wamewakamata wanajeshi 40 lakini hata hivyo wanamgambo 30 wa Taliban nao pia wameuawa.
Mashambulizi ya wanamgambo wa Taliban kaskazini mwa Afghanistan yanakuja katika kipindi ambacho mamia wameuawa pamoja na kujeruhiwa katika jimbo la Ghazni Kaskazini Magharibi nchini humo lililoko katika barabara kuu inayounganisha mji wa Kabul na upande wa kusini mwa nchi hiyo.
Wakazi waliolazimika kuukimbia mji wa Ghazni wanasema wanamgambo wa Taliban wamekata mawasiliano, umeme na huduma za maji huku hospitali zikianza kupungukiwa dawa na maduka pamoja na majumba kadhaa yakiwemo ya serikali yameharibiwa.
Hayo yanajiri mnamo wakati maafisa wa Afghanistan wakidai vikosi vya usalama vimewarejesha nyuma wanamgambo wa Taliban kutoka jimbo la Ghazni na kuwa sasa wanajaribu kuwaondoa kabisa katika maeneo ya pembezoni mwa mji huo.
Nasart Rahimi msemaji wa wizara ya mambo ya ndani anasema vikosi vya usalama hapo jana vilikuwa vikiendelea kuwasaka wanamgambo wa Taliban katika kila sehemu walipo huku msemaji wa vyombo vya habari vya kijeshi akisema helikopta za jeshi zilikuwa zikisaidia katika operesheni ya ardhini.
Hata hivyo msemaji wa wanamgambo wa Taliban Zabihullah Mujahdid anakanusha kuwa wanamgambo hao wameondolewa katika jimbo la Ghazni na kusisitiza mapigano bado yanaendelea.
Umoja wa Mataifa wataka haki za binadamu ziheshimiwe
Wakati huohuo Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya raia 100 wameuawa tangu mapambano hayo ya Ghazni yalipoanza Alhamisi iliyopita na kuzitaka pande zinazohusika na mgogoro nchini humo kuheshimu sheria zinazohusiana na haki za binadamu.
Mashambulizi hayo mapya ya Taliban yanakuja ikiwa ni mwaka mmoja tangu utawala wa rais wa Marekani Donald Trump ulipoanzisha mkakati wake nchini Afghanistan mnamo wakati wanamgambo wa Taliban wakiendelea kujiimarisha katika uwanja wa mapambano licha ya maafisa wa Marekani kuonesha matumaini ya kupatikana amani nchini humo.
Hatua hii inazidi kuibua maswali juu ya uwezekano wa Marekani wa kukomesha mapigano nchini Afghanistan.
Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imetangaza Jumatatu wiki hii kuwa afisa wa kijeshi wa nchi hiyo Reymond Rarogal mwenye umri wa miaka 36 amefariki Jumapili iliyopita kufuatia majeraha aliyoyapata wakati wa operesheni iliyofanyika katika jimbo la Helmand.
Kutokana na kurejea tena kwa mashambulizi ya kundi la Taliban nchini Afghanistan baadhi wanahoji iwapo Rais Trump atafikia hatua ya kushindwa kujihusisha kijeshi nchini humo ambapo Marekani inatumia dola bilioni 4 kwa mwaka ili kuviongezea nguvu kijeshi vikosi vya Afghanistan.
Mwandishi: Isaac Gamba/APE/RTRE
Mhariri: Bruce Amani