Wanamaji wa Ujerumani kulinda fukwe za Somalia
11 Desemba 2008
Uamuzi wa kutumwa jeshi la wanamaji wa Ujerumani kuwashinda nguvu maharamia na mswaada wa sheria wa kinga ya data za raia ndizo mada kuu zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.
Tuanze lakini na uamuzi wa kupelekwa jeshi la wanamaji wa Ujerumani katika fukwe za Somalia.Gazeti la WIESBADENER KURIER linahisi uamuzi huo ni wa maana,na kuendelea kuandika:
Ujerumani isiyokua na mali ghafi na ambayo shughuli zake za kiuchumi zinaegemea zaidi biashara ya nje,haina abudi isipokua kutegemea njia huru za kibiashara-Ingekua kichekesho na wala isingeaminika kama Ujerumani ingepinga kujiunga na mpango wa umoja wa ulaya wa kupambana na visa vya maharamia katika fukwe za Somalia.Chupu chupu wamefanikiwa washirika wa serikali ya muungano wa vyama vikuu,kuachana na malumbano yao kuhusu suala kama inaruhusiwa kikatiba au la kutumwa wanajeshi wa Ujerumani kupambana na maharamia."
Gazeti la VOLKSSTIMME la mjini Magdeburg linafurahikia kwamba wanamaji hao wana haki ya kutumia nguvu kutekeleza jukumu lao.Gazeti linaendelea kuandika:
"Hadi wakati huu wanajeshi wa kijerumani waliruhusiwa kutumia silaha kama njia ya mwisho ya kujihami.Hivi sasa lakini wanaweza kuwaandama na kuwakamata,kama hawajatoroka.Suala jengine lakini linazuka hapo nalo ni jee maharamia watakaotiwa mbaroni watafanywa nini?Watabidi wafikishwe mahakamani.Lakini wapi?Hicho ndo kitandawili cha jukumu hilo.Kuwaachia tuu katika fukwe za Somalia,kama hakuna nchi itakayokubali kuwafikisha mahakamani,haitakua na maana yoyote kwasababu maharamia hao hao watapata moyo na kuendelea upya na hujuma zao.
Gazeti la MÜNCHNER MERKUR linashuku kama shughuli za kuhakikisha usalama wa safari za meli katika fukwe za Somalia,zitafanikiwa.
"Kwa wakati wote ule ambapo wananchi fukara wa Somalia hawatakua na matumaini ya kuboreka hali yao ya maisha,na takriban kila siku wakishuhudia jinsi neema ya dunia inavyowapita na kuelekea mahala kwengine,basi nao maharamaia hawatasitisha visa vyao.Hapa linazuka suala mpaka lini shughuli hizo za wanamaji zitaendelea.Kwasababu bila ya kupatiwa jibu suala la Somalia yenyewe kuna uwezekano mkubwa shughuli hizo huenda zikadumu milele.
Gazeti la NORDKURIER la mjini NEUBRANDENBURG linajiuliza kama yote haya yanaambatana na katiba.Gazeti linaendelea kuandika:
"Sheria msingi imetaja wazi wazi kabisa,wanajeshi wa Ujerumani jukumu lao ni kuihami nchi hii tuu.Mijadala yote haisaidii kitu.Kinachohitajika hapa ni marekebisho ya katiba.Marekebisho hayo yatabidi yafafanue kwaanini wanajeshi wa Ujerumani watumikie nchi za nje.Kama ni kwaajili ya kuhifadhi masilahi ya kimkakati ya Ujerumani na kadhalika"