Wanakoishi matajiri wakubwa wa Kiafrika
Katika nchi nyingi za Kiafrika za kusini mwa jangwa la Sahara umasikini ni tatizo kubwa lakini kulingana na ripoti ya taasisi ya New World Wealth, idadi ya mamilionea katika nchi hizi inaongezeka. Nazo ni:
Afrika Kusini
Nchi ya Kiafrika iliyo na idadi kubwa kabisa ya mamilionea ni Afrika Kusini. Kuna matajiri wa hali ya juu 46,800 wanoishi baina ya miji ya Cape Town na Johannesburg - na bado wanatarajiwa kuengezeka. Ikilinganishwa idadi hiyo na barani Ulaya, nchini Uingereza kwa sasa kuna mamilionea 840,000.
Nigeria
Kulingana na gazeti la Forbes, mtu tajiri kabisa barani Afrika ni Mnigeria: Aliko Dangote. Alitengeneza utajiri wake - kwa sasa ni taktiban bilioni 18.2 za Kimarekani- kupitia biashara za vyakula, saruji na madini. Dangote ni mmoja wapo wa matajiri 15, 400 walioko nchini Nigeria, ambayo pia ni miongoni mwa nchi kuu za Afrika wanakotokea wakimbizi wanaokimbilia barani Ulaya.
Kenya
Utajiri jumla wa mamilionea wote 8500 wa Kenya,sawa na thuluthi mbili ya uchumi wa taifa hilo - ni uwiano mkubwa sana. Wengi wao wana vitega uchumi katika viwanda na kilimo cha bustani. Kwa wastani, tajiri wa Kenya ana fedha za thamani ya dola milioni 83 za Kimarekani, lakini bado karibu nusu ya wananchi wa taifa hilo wanaishi maisha ya kimasikini ya dola mbili kwa siku.
Angola
Kutokana na biashara ya mafuta Angola kwa sasa ina matajiri wa hali ya juu 6, 400, idadi hii imezidi mara sita na ilivyokuwa miaka 15 iliyopita. Angola pia ndipo anapotokea mwanamke tajiri kabisa Afrika: Isabel dos Santos, ambaye ni binti wa rais wa nchi hiyo Jose Edurado dos Santos. Utajiri wake unakadiriwa kuwa ni dola bilioni 3.2 za Marekani.
Mauritius
Idadi ya watu katika kisiwa cha Mauritius ni milioni 1.3, na bado kuna mamilionea 3,200 wa dola. Sekta ya utalii kisiwani humo imeshamiri, na ina sifa kama mfano wa kuigwa katika utozaji kodi wa sekta ya utalii. Hata hivyo, kulingana na Benki Kuu ya Dunia, tatizo la ukosefu wa usawa baina ya binaadamu linaongezeka kisiwani humo na uchumi pia unahitaji kupanuliwa katika sekta nyenginezo.
Namibia
Sekta ya uchimbaji wa madini namibia inachangia asilimia 25 ya uchumi wa nchi hiyo, na almasi ndio bidhaa yake kuu inayosafirishwa nje ya nchi. Nchi hiyo ina idadi ya watu milioni mbili tu, na Wanamibia 3,100 baina yao wanamiliki utajiri wa zaidi ya dola milioni moja. Kipato cha kila mtu nchini humo ni cha kiwango cha juu, lakini mgawanyo wa pato zima la Namibia umekosa usawa.
Ethiopia
Ethiopia hivi karibuni tu ndio ilijiunga katika orodha ya nchi kumi zenye matajri wakubwa wa nchi za Afrika kusini mwa jangwa la Sahara. Utulivu wa kisiasa pamoja na uwekezaji wa kigeni umepelekea kupatikana kwa ukuwaji wa kiuchumi uliotulia tangu mwaka 2003. Ikiwa Waethiopia 2,800 sasa wanaweza kujiita matajiri wakubwa nchini humo, thuluthi moja ya idadi nzima ya watu bado inaishi katika ufukara.
Ghana
Dhahabu, mafuta na kakao ni bidhaa muhimu kabisa Ghana zinazosafirishwa nje ya nchi. taifa hilo la magharibi mwa bara la Afrika ina mamilionea takriban 2,700 kwa sasa. Mara nne ya idadi ilokuwa nayo mwanzo mwa Milenia. Mbali na bidhaa hizo, matajiri nchini Ghana pia wanategemea biashara ya huduma za kifedha pamoja na ya mali isiyohamishika.
Botswana
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Dunia, Botswana ni nchi ya kupigiwa mfano kimaendeleo. Kwa miongo kadhaa kiwango cha ukuwaji kimebaki kuwa imara. Nchi hiyo ina mamilionea 2,600, wengi wao wamewekeza katika sekta ya almasi. Hata hivyo, umasikini bado ni tatizo, zaidi ni kutokana na idadi kubwa ya watu walioambukizwa virusi vya ukimwi pamoja na ukosefu wa ajira. .
Côte d'Ivoire
Miaka minane iliyopita, vita vya wenyewe kwa wenyewe Côte d'Ivoire vilimalizika, na tangu wakati huo imeweza kufurahia uchumi ulio imara. Kuna mamilionea 2,300 wanaoishi nchini humo, idadi hiyo pia inatarajiwa kuongezeka zaidi katika miaka michache ijayo. Lakini, Côte d'Ivoire bado inashika nafasi ya 171 kati ya nchi 187 katika Orodha ya Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo .