1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Ufaransa wapata pigo kubwa Afghanistan

Nijimbere, Gregoire20 Agosti 2008

Katika kitendo cha shambulio la wapiganaji Wataliban nchini Afghanistan, wanajeshi wa Ufaransa wameuawa na wengine kujeruhiwa. Ufaransa inasema itaendelea na shughuli zake za kulinda amani huko Afghanistan.

https://p.dw.com/p/F1Gy
Wanajeshi wa kigeni wakikabiliana na shambulio la Wataliban huko Afghanistan, mkoa wa HermandPicha: picture-alliance/ dpa

Wanamgambo Wataliban walivizia magari ya kijeshi ya Ufaransa katika eneo la bonde na kufanya shambulio lisilotarajiwa. Katika hatua ya kwanza ya mapigano yaliyofuatia, wanajeshi wawili wa Ufaransa walifariki pao hapo lakini kwa jumla, ni 10 waliyouawa katika mapigano hayo yaliyodumu masaa matano. Inaarifiwa wanajeshi wengine 21 wamejeruhiwa katika shambulio hilo la kuvizia lililofanywa na waasi Wataliban nchini Afghansitan.

Hiyo ndio idadi kubwa ya wanajeshi wa kigeni kuwahi kuuawa wakati moja tangu kuanguka utawala wa kitaliban mnamo mwaka wa 2001.

Jeshi la kimataifa la kulinda amani nchini Afghanistan, limekataa kutoa maelezo kamili juu ya shambulio hilo na kusema tu kuwa mapigano yametokea masafa ya kilomita 50 mashariki mwa mji mkuu Kabul.

Takriban wapiganaji wa kitaliban 13 wameuawa kwenye mapigano hayo baada ya ndege za kijeshi kuingilia kati.

Rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, amesisitiza kwamba Ufaransa itaendelea kupambana na ugaidi na ujumbe wake wa kulinda amani nchini Afghansitan utaendelea.

Rais Nicolas Sarkozy tayari amewasili nchini Afghansitan ambako anatarajiwa kuwatembelea wanajeshi wa Ufaransa katika kudhihirisha uungwaji wake mkono baada ya mauaji hayo kutokea.

Upande wa jeshi la Ufaransa, mauaji hayo ya hapo jana nchini Afghanistan ni pigo kubwa na ndio mauaji mabaya kuwahi kutokea kwa wanajeshi wa Ufaransa tokea ujumbe wa kuweka amani wa Ufaransa nchini Lebanon mwaka wa 1983.