1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Nigeria wakimbilia Cameroon

26 Agosti 2014

Kundi la Boko Haram hapo jana limeuvamia mji mmoja wa mpakani kaskazini mashariki mwa Nigeria, na kuwalazimu wakaazi na wanajeshi kutoroka na kuingia katika nchi jirani ya Cameroon wakiwemo wanajeshi

https://p.dw.com/p/1D18f
Nigeria Soldaten
Picha: AFP/Getty Images

Tukio hilo ni ishara ya karibuni kuwa wanamgambo hao wenye itikadi kali za kiislamu wana uwezo wa kushambulia wakati wowote wanaotaka bila kupata upinzani wowote kutoka kwa vyombo vya serikali.

Shambulizi hilo la Gamboru Ngala limekuja baada ya mji huo kuharibiwa vibaya katika shambulizi jingine la mwezi Mei mwaka huu ambalo lilisababisha vifo vya watu 300 na kuzusha kilio na hasira kutoka kwa umma baada ya jeshi kushindwa kuwaokoa raia.

Shambulizi la jana, limewalazimu wakaazi wengi wa mji huo kutafuta hifadhi katika mji wa kaskazini ya Cameroon, Fotokol, ambako wanameshi wa ulinzi wa mpakani wa Cameroon walitumwa ili kuimarisha usalama.

Kamerun Soldaten gegen Boko Haram
Wanajeshi wa Cameroon wameimarisha ulinzi wa mpakaniPicha: Reinnier KAZE/AFP/Getty Images

Wanajeshi wa Nigeria ni miongoni mwa waliohamia nchini humo, kwa mujibu wa duru za kijeshi za Cameroon, ambazo zimesema zaidi ya wanajeshi 450 wa Nigeria walitoroka kutoka kwenye vituo vyao siku ya Jumapili katika jimbo la Borno kwa kuhofia mashambulizi ya Boko Haram.

Jeshi la Nigeria hata hivyo limepuuzilia mbali madai hayo na kusisitiza kuwa majeshi yake yaliingia maeneo ya mipakani kama mbinu ya kujipanga upya wakati walijikuta katika ardhi ya Cameroon. Baadhi ya wakaazi waliofanikiwa kuvuka mpaka wamesema wanamgambo wameukamata mji wa Gamboru Ngala baada ya makabiliano makali hali iliyowafanya wakaazi walioingiwa na hofu kujifungia majumbani.

Mjini Fotokol, wakaazi pia wameripoti kusikia milio ya risasi. Mbinu wanayotumia sasa Boko Haram ya kuiteka miji ni tofauti na mbinu zake za awali ambapo walifanya mashambulizi ya kuwalenga na kuwauwa raia na kuchoma moto miji na vijiji. Kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau alisema mwishoni mwa wiki katika video iliyopatikana na shirika la habari la AFP kuwa mji wa Gwoza, kusini magharibi mwa Gamboru Ngala, sasa chini ya utawala wa Kiislamu. Jeshi la Nigeria limepuuzilia mbali madai ya Shekau kama ni maneno matupu, na kusisitiza kuwa uhuru wa nchi unasalia kama ulivyo.

Nigeria Boko Haram Abubakar Shekau Archiv
Kiongozi wa Boko Haram Abubakar ShekauPicha: picture alliance/AP Photo

Watalaamu wanaamini kuwa Boko Haram itajaribu kuikamata miji zaidi katika jimbo hilo wakati jeshi la Nigeria likishindwa au likikataa kuwakabili. Baadhi ya wanajeshi wa Nigeria katika mji wa Maiduguri wamekataa kuingia mapambano ya kuukomboa mji wa Gwoza kwa sababu ya kile wanasema kuwa ni silaha hafifu ambazo zinawaweka hatarini mikononi mwa waasi ambao wana silaha nzito na za kisasa kuliko walizo nazo.

Watalaamu wa ulinzi pia wanahoji kuwa Nigeria inahitaji kuimarisha mkakati wake wa kupambana na uasi na kutumia mbinu ya mapigano ya chini kwa chini, badala ya kutegemea mbinu za kawaida. Wengine wanalalamika ukosefu wa nia ya kisiasa ili kupambana na donda la Boko Haram, wanaotaka kuunda Dola la Kiislamu na ambao harakati zao zinalenga shule, makanisa na ofisi za serikali.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Josephat Charo