1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Marekani wakamilisha harakati za kijeshi nchini Iraq

Oumilkher Hamidou31 Agosti 2010

Rais Barack Obama ataahutubia taifa leo usiku kuadhimisha mwisho wa shughuli z kijeshi za nchi yake nchini Iraq

https://p.dw.com/p/P05b
Mlolongo wa vifaru na magari ya kijeshi ya Marekani yanaelekea Kuweit baada ya kuihama IraqPicha: AP

Wanajeshi wa Marekani wanajiandaa kukamilisha harakati zao za kijeshi hii leo nchini Iraq katika wakati ambapo makamo wa rais Joe Biden anakutana na viongozi wa nchi hiyo iliyoteketezwa kwa vita mjini Baghdad,miaka sabaa baada ya mapigano yaliyogharimu maelfu ya maisha.

Watabakia wanajeshi 50 elfu tuu nchini Iraq watakaokua na jukumu la kuwapatia mafunzo vikosi vya usalama na polisi hadi mwishoni mwa mwaka 2011.

Uamuzi wa kumaliza shughuli za kijeshi za Marekani nchini Iraq unatekelezwa katika wakati ambapo bado hakuna serikali iliyoundwa nchini humo baada ya uchaguzi wa bunge ulioitishwa Machi mwaka huu na matumizi ya nguvu yanazidi wakilengwa pia wanajeshi na polisi.

"Kwa ufupi, tumedhamiria kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu pamoja na serikali na umma wa Iraq, lakini kwanza panahitajika mshirika ili kuweza kuwa na ushirikiano" amesema hayo Tony Blinken ambae ni mshauri wa masuala ya usalama wa makamo wa rais wa Marekani Joe Biden,aliyewasili jana mjini Baghdad.

Hii leo makamo wa rais wa Marekani, Joe Biden, amepanga kukutana na viongozi wa kisiasa mjini Baghdad. Suala la kuundwa serikali ni miongoni mwa mada makamo wa rais wa Marekani anazopanga kuzungumzia.

Kesho makamo wa rais wa Marekani atahudhuria sherehe za kuanzishwa opereshini iliyopewa jina "Ukurasa mpya"-ambapo wanajeshi wa Marekani watakua wakisaidia na kutoa ushauri nchini Iraq.

Barack Obama Präsident Atlanta Irak Abzug
Rais Barack Obama anapanga kuwahutubia wamarekani baadae leio usikuPicha: AP

Mjini Washington rais Barack Obama anapanga baadae leo usiku kulihutubia taifa kuadhimisha siku ya kuondoka rasmi wanajeshi wa Marekani kutoka Iraq. Kabla ya hapo rais Obama anapanga kuwatembelea wanajeshi waliorejea kutoka Iraq,walioko katika kituo cha kijeshi cha Texas kusini mwa nchi hiyo.

Ahadi ya kuwarejesha nyumbani wanajeshi wa Marekani aliitoa tangu mwaka mmoja na nusu uliopita alipotamka:

"Hatuwezi kupiga doria milele katika barabara za Iraq, hadi watakapojisikia salama na hatuwezi pia kubakia hadi Umoja kamili wa Iraq utakapopatikana."

Katika hotuba yake baadae leo usiku, rais Barack Obama anatazamiwa kuwashukuru na kuwasaifu wanajeshi wa Marekani wanaolinda amani nchini Iraq. Wanajeshi zaidi ya milioni moja walipelekwa Irak tangu mwaka 2003 na takriban 4400 wamepoteza maisha yao nchini humo.

Viongozi wa Iraq wameelezea wasi wasi wao kutokana na kumalizika rasmi shughuli za kijeshi za wanajeshi wa Marekani. Mashambulio ya waasi yamezidi kushika kasi miezi ya hivi karibuni.

Jana usiku pia waasi hawakuchelea kufyetua makombora mawili katika eneo la kijani- zoni inayolindwa vikali kati kati ya mji mkuu wa Baghdad kunakokutikana wizara muhimu pamoja na ofisi za mabalozi, ikiwa ni pamoja na ile ya Marekani.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/ Afp,Reuters

Imepitiwa na :Othman Miraji