Wanajeshi wa Marekani kuendelea kubakia Afghanistan
16 Oktoba 2015Serikali ya Afghanistan imeupokea uamuzi wa Marekani kuwabakisha maelfu ya wanajeshi wake nchini Afghanistan baada ya mwaka 2016.
Uamuzi wa rais Barack Obama uliotangazwa alhamisi wa kuwabakisha wanajeshi 9800 wa Marekani nchini Afghanistan umekuja katika wakati ambapo amekiri kwamba vikosi vya Afghanistan havijakuwa tayari kusimama peke yake kukabiliana na hali ya ukosefu wa usalama.Rais Obama ameutaja mpango huo kama hatua mwafaka inayohitajika kutokana na kutokuwa imara kwa wanajeshi wa Afghanistan.
Kadhalika Obama amesisitiza kwamba yeye kama kamanda wa majeshi ya taifa lake hawezi kuruhusu Afghanistan kutumiwa kama eneo salama na magaidi kuendesha mashambulizi yao dhidi ya Marekani kwa mara nyingine.Uamuzi wa Obama ulitangazwa moja kwa moja kupitia televisheni.Kwa upande wake Afghanistan imeridhika na uamuzi huo wa Marekani ambapo serikali imetoa taarifa alhamisi usiku inayosema kwamba itakabiliana na kitisho pamoja na magaidi kwa nguvu zote,ingawa pia imeongeza kusema kuwa itaacha wazi milango ya kukaribisha mazungumzo ya amani.
Rais Ashraf Ghani pia ametuma ujumbe kupitia mtandao wa Twitter akiunga mkono kikamilifu uamuzi wa Obama.Katika ujumbe huo rais Ghani amesema mbali na kuimarisha usalama na maendeleo ya nchi yake bado wana ari zaidi kuliko ilivyokuwa awali ya kuimarisha uhusiano katika suala zima la kupambana na ugaidi .Ikumbukwe kwamba kuongezeka kwa mapambano hivi karibuni kumeonesha umuhimu zaidi wa dhima ya wanajeshi wa Marekani katika kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Afghanistan pamoja na kusimamia operesheni za kukabiliana na ugaidi.
Wiki mbili zilizopita wanamgambo wa kundi la Taliban walipata ushindi mkubwa wa kijeshi tangu kushuhudiwa uvamizi ulioongozwa na Marekani nchini humo mwaka 2001 ambapo waliuteka mji wa Kunduz.Hata hivyo hatua za kujibu mashambulizi zilizochukuliwa na vikosi vya kijeshi vya Afghanistan vikisaidiwa na wanajeshi wa Marekani na Jumuiya ya kujihami ya NATO zilichangia hatimae wanamgambo hao kurudi nyuma.
Ni wiki hii ambapo pia vikosi vya NATO vilisema wanajeshi wa Marekani na Afghanistan walifabnya operesheni kadhaa za kijeshi kusini mwa mkoa wa Kandahar na kuharibu ngoma ya wamgambo wa alqaeda katika eneo hilo.Na kutokana na uamuzi wa Marekani wa kuendelea kubakisha wanajeshi wake katika taifa hilo wanamgambo hao wamesema wataendelea na mapambano hadi wanajeshi wote wa Marekani waondoke.
Msemaji wa Taliban Zabiullah Mujahid amesema,ninamnukuu''Ni Wamarekani walioamua kuivamia Afghanistan.lakini ni sisi tutakaoamua lini wataondoka,Mashambulizi yakiwazidia na watakapoona wanatumia kiasi kikubwa cha fedha kugharimia vita visivyokuwa na maana watalazimika kubadilisha sera zao za ukandamizaji.Vita vyetu vitaendelea hadi wavamizi wote watakapoondoka''Mwisho wa kauli ya msemaji wa Taliban.
Alipoingia madarakani rais Obama mwaka 2009 aliahidi kumaliza vita nchini Iraq na Afghanistan lakini zaidi ya miaka 6 imepita maelfu ya wanajeshi wake bado wako katika nchi zote mbili.Na ukweli wa mambo ni kuwa vita vya Afghanistan vimesababisha vifo vya zaidi ya wanajeshi 2000 wa Marekani na maelfu ya wengine wamejeruhiwa. Vita vya Afghanistan vilichochewa na hatua ya Taliban kukataa kuwakabidhi kwa Marekani viongozi wa Alqaeda akiwemo Osama Bin Laden baada ya mashambulizi ya Septemba 11 dhidi ya Marekani.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman