Wanajeshi wa Mali wakubali kuondoka madarakani
7 Aprili 2012Tangazo la makubaliano hayo limekuja saa chache tu baada ya waasi wanaopigania kujitenga kwa eneo la Kaskazini mwa Mali kujitangazia uhuru wa eneo hilo, hatua ambayo imeufanya mzozo wa nchi hiyo kuwa mgumu zaidi.
Siku ya Ijumaa (6 Aprili 2012) Kapteni Sanogo alijitokeza kutoka ofisini kwake katika kambi ile ile ya kijeshi ambapo uasi ulianza na ambapo palianza kuchukuwa nafasi ya kuwa makao makuu ya serikali tangu mapinduzi ya Machi 21, na kutangaza kwamba amekubali kusaini makubaliano ya kuachia madaraka.
Akiwa amezungukwa na mawaziri wa nchi jirani, Kapteni Sanogo alisoma makubaliano hayo, akisema kwamba chini ya Kifungu Namba 36 cha katiba ya Mali, mkuu wa bunge la taifa anakuwa rais wa mpito katika wakati ambapo pana ombwe la uongozi. Mkuu huyo wa bunge ataunda serikali ya mpito ambayo itafanya uchaguzi mpya.
"Katika hali ambapo nafasi ya rais wa jamhuri ni tupu kwa sababu yoyote iwayo, kazi za rais wa jamhuri zitachukuliwa na raisi wa bunge la taifa." Alisema Kapteni Sanogo.
ECOWAS yaondoa vikwazo dhidi ya Mali
Ingawa makubaliano hayo hayakusema lipi litakuwa jukumu la wanajeshi waliofanya mapinduzi hapo baadaye, hata hivyo vikwazo vyote vilivyowekwa na Jumuiya ya Uchumi ya Afrika ya Magharibi (ECOWAS) vitaondolewa mara moja.
Makubaliano hayo hayakusema pia ni lini mkuu huyo wa bunge la taifa, Dioncounda Traore, ataanza kushikilia wadhifa wa urais wa muda na wala siku ya kuanza kwa kipindi cha mpito kuelekea uchaguzi mpya. Traore aliikimbia nchi baada ya mapinduzi.
Ingawa kifungu cha 36 cha katiba kinataka uchaguzi ufanyikendani ya siku 40, makubaliano yanasema kwamba muda huo unaweza kuongezwa kutokana na uasi wa Kaskazini ambao umelifanya eneo hilo ambalo ni kubwa zaidi kuliko sehemu ya Mali iliyobakia kuwa uwanja wa kivita.
"Kwa sababu ya mazingira yasiyo ya kawaida ambayo kwa sasa nchi yetu inapitia, kwa sababu ya mgogoro wa taasisi za serikali na uasi wa silaha wa kaskazini ambao umeathiri vibaya utendaji kazi za jamhuri na kwa sababu ya kutokuwezekana kuandaa uchaguzi ndani ya siku 40, kama inavyotakiwa na katiba, ni vyema kuandaa kwanza kipindi cha mpito cha kisiasa kwa lengo la kuandaa uchaguzi huru, wa kidemokrasia na wa uwazi." Alisema Kapteni Sanogo.
Tangazo hili lilikaribishwa vyema na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso, Djibrill Bassole, ambaye alimsindikiza Kapteni Sanogo wakati wa kuyasoma makubaliano. Bassole alisema baadaye kuwa mataifa jirani yamekubali kuondoa vikwazo vyote vilivyoanza mapema wiki hii, vikiwemo vya kufunga mipaka ya Mali.
Nchi hiyo ambayo haina mpaka wa bahari, inaingiza mafuta yake yote kutoka nje na tayari wakaazi wa mji mkuu, Bamako, walishaanza kukosa huduma ya umeme.
Jumuiya ya kimataifa haina uhakika
Afisa mmoja wa ngazi za juu, ambaye alihusika katika mazungumzo yaliyozaa mapatano haya, amesema kwamba mkuu wa bunge la taifa huenda angelirudi nchini Mali Jumamosi kwa ndege. Afisa huyo alisema kwamba Kapteni Sanogo, ambaye hadi karibuni tu "alikataa katakata kuachia madaraka, hatimaye ameamua kuirudisha nchi katika utaratibu wa kidemokrasia."
Mwanadiplomasia mmoja wa Magharibi mjini Bamako amesema, hata hivyo, kwamba ingawa anatarajia kila jambo kwenda vyema, bado anahofia Kapteni Sanogo anaweza kugeuza mawazo yake.
"Tunapaswa kuchukuwa msimamo wa kusubiri na kuona. Nataraji iwe ni kweli na kwamba nchi inarudi katika utawala wa kiraia ili Mali iweze kusimama tena kwa miguu yake." Alisema mwanadiplomasia huyo aliyekataa kutajwa jina lake.
Habari ya Kapteni Sanogo kukubali kusaini makubaliano ya kuondoka madarakani zilikuja saa chache tu baada ya waasi wa Tuareg, ambao walichukuwa udhibiti wa eneo la kaskazini baada ya machafuko yaliyotokana na mapinduzi, kujitangazia uhuru.
ECOWAS yapanga kuwavamia waasi wa Tuareg
Nchini Cote d'Ivoire, wakuu wa kijeshi wa mataifa 13 jirani ya Mali walikutana kupanga uingiliaji kati kijeshi ili kuwarudisha nyuma waasi wa kaskazini. Jamii ya Tuareg wamekuwa wakipigania uhuru wao tangu mwaka 1958, pale viongozi wao walipomuandikia barua rais wa Ufaransa kutaka watawala hao wa kikoloni kutenga taifa tafauti la jamii yao kwa jina la Azawad kwa lugha ya Kituareg.
Lakini badala yake eneo kaskazini, ambalo linakaliwa na watu wa jamii ya Tuareg ambao ni weupe, likafanywa kuwa sehemu moja ya nchi na eneo la kusini, ambako kunakaliwa na watu weusi, na ambao wana udhibiti wa mji mkuu na fedha za nchi.
Kundi lililojitangazia uhuru wa Azawad hapo Ijumaa linafuata siasa zinazotenganisha siasa na dini, lakini walisaidiwa na kundi la Kiislamu linalojaribu kuweka utawala wa Shariah katika eneo hilo lenye msimamo wa kati, ukiwemo mji wa kihistoria wa Timbuktu.
Tayari Umoja wa Afrika, Umoja wa Ulaya, Marekani na, zaidi, mkoloni wa zamani, Ufaransa, wameshakataa kuutambua uhuru huo wa Azawad. Ufaransa imefikia umbali wa kuahidi kutoa msaada wa kifedha na vifaa kwa kikosi cha wanajeshi wa jumuiya ya ECOWAS, ikiwa jumuiya hiyo itaamua kuanzisha operesheni ya kijeshi dhidi ya waasi wa Tuareg.
Wakati wa kuchukuwa madaraka, Kapteni Sanogo na wenzake walisema walifanya hivyo kwa sababu ya Rais Amadou Toumani Toure kushindwa kuushughulikia uasi wa kaskazini ulioanza mwezi Januari.
Mgogoro huo umegharimu vifo kadhaa vya wanajeshi wa Mali, na katika makubaliano yaliyosainiwa hapo Ijumaa kuna kipengele kinachotaka kulipwa fidia kwa familia za wanajeshi waliouawa kwenye vita hivyo. Makubaliano hayo pia yanatoa kinga kamili kwa wanajeshi walioshiriki kwenye mapinduzi.
Hata hivyo, lililobaki bila kujibiwa ni jaala ya rais aliyeondoshwa madarakani, Toure, ambaye alikimbilia mafichoni na taarifa zake hazijuilikani kikamilifu. Bassole aliwaambia waandishi wa habari baada ya kuyasoma makubaliano hayo kwamba mataifa jirani ya Mali yameomba kwamba Toure aruhusiwe kurudi.
"Tumeeleza hamu yetu ya kumuona Rais ATT akiruhusiwa kurudi nyumbani akiamua mwenyewe na kwamba usalama wake uthibitishwe na vikosi vya ulinzi na usalama," alisema Bassole.
Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/AP
Mhariri: Bruce Amani