Wanajeshi wa Mali wakataa mpango mpya wa ECOWAS
29 Aprili 2012Kukataa huko kwa wanajeshi kumezua ukungu wa shaka katika makubaliano ya mwezi uliopita ya kutatua mkwamo wa kisiasa nchini humo.
Mwanzoni wanajeshi hao walikubali kurudishwa kwa utawala wa kiraia ndani ya siku 40 kwa serikali ya muda inayoongozwa na Rais Dioncouda Traore na kisha kuiruhusu nchi kufanya uchaguzi mwishoni mwa mwezi Mei.
Lakini hapo Alhamis (26 Aprili), ECOWAS ilisema kuwa serikali ya mpito ni lazima ipewe hadi miezi 12 kuweza kutayarisha uchaguzi. Wanajeshi sasa wanaishutumu ECOWAS kwa kufanya maamuzi bila ya kuwashirikisha wao, huku wakisema kuwa mabadiliko hayo yatauathiri utaratibu mzima wa kipindi cha mpito.
"Ninataka kuthibitisha tena kwa kila mtu kwamba baraza la kijeshi litabakia tu na makubaliano ya mwanzo ya siku 40 lililosaini na ECOWAS. Haiwezekani kubadilisha." Alisema kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi, Kapteni Amadou Sanogo baada ya mkutano muhimu na wapatanishi wa ECOWAS.
"Hili ni kuhusiana na utawala wa muda wa Dioncounda. Baada ya siku 40 tutaamua taasisi ipi ya dola itaendelea. Hayo ndiyo tuliyokubaliana na hayawezi kubadilishwa," Sanogo aliwaambia waandishi wa habari ambaye, hata hivyo, hakutaja kuhusu kufanyika kwa uchaguzi baada ya kipindi cha siku 40.
Wanajeshi waipinga ECOWAS
Wanajeshi wenye silaha walikusanyika nje ya kambi ya jeshi ya Kati ulikokuwa ukifanyika mkutano baina ya Sanogo na wajumbe wa ECOWAS, wakipiga mayowe ya kuipinga ECOWAS na kiongozi wa mpito, Dioncounda.
Tangu mwanzo ilikuwa imeonekana kwamba ni jambo lisilo rahisi kwa Mali kutekeleza ahadi yake ya kufanya uchaguzi ndani ya siku 40, hasa baada makundi ya Kiislamu na waasi wanaopigania kujitenga kutumia fursa ya mapinduzi ya kijeshi kwa kuteka na kujitangazia uhuru wa eneo la kaskazini.
Kutajwa kwa rais wa muda kuliondosha madaraka kutoka kwa wanajeshi kwenda kwa kiongozi wa kiraia, lakini bado wanajeshi ndio wanaoonekana kuwa na nguvu katika taifa hilo masikini la magharibi ya Afrika.
Tayari wanajeshi hao wamesema haukubaliani na mpango mwengine wa ECOWAS wa kupeleka wanajeshi nchini Mali na kwamba watawachukulia wanajeshi wowote wa kigeni kama maadui.
Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Stumai George