1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi wa Iraq wadhibiti mji wa Kirkuk

17 Oktoba 2017

Maelfu ya raia wamerudi katika mji wa Kirkuk huko Iraq siku moja baada ya kuyakimbia makaazi yao wakati ambapo kikosi cha wanajeshi wa Iraq kimewaondoa wanajeshi wa Kikurdi kutoka eneo hilo lenye utajiri wa mafuta.

https://p.dw.com/p/2lxau
Irak Regierungstruppen in Kirkuk
Picha: picture-alliance/AA/A.M. Garip

Raia hao wamerejea katika mji huo wakipitia barabara kuu kuelekea mashariki mwa mji huo. Wanajeshi wa Kikurdi walikuwa wameweka kizuizi pamoja na magari ya kijeshi, lakini walikuwa wanawakubalia raia kurudi mjini humo huku wengi wao wakionekana wamewabeba watoto na mali zao kwenye magari.

Haya yanakuja baada ya kikosi cha Iraq kupitia afisa mmoja mkuu wa kijeshi kutangaza kuwa kimekamilisha operesheni ya kuchukua udhibiti wa visima vyote vya mafuta vinavyosimamiwa na kampuni inayomilikiwa na serikali katika eneo hilo la Kirkuk. Wanajeshi wa Iraq wamevidhibiti visima vya Bai Hassan na Avana kaskazini magharibi mwa Kirkuk.

Visima hivyo hapo awali vilikuwa vinashikiliwa na kikosi cha usalama cha Wakurdi wanaojulikana kama Peshmerga lakini wameondoka katika eneo hilo baada ya shinikizo hilo la kikosi cha Iraq.

Umoja wa Mataifa wataka pande zote kusitisha mapigano

Kutumwa kwa kikosi hicho cha Iraq katika eneo la Dibis ambapo ndipo kuliko na hivyo visima vya Bai Hassan na Avana, ni kati ya operesheni iliyoamrishwa na Waziri Mkuu Haider al-Abadi, aliyetaka maeneo yanayoshikiliwa na Wakurdi yadhibitiwe.

USA Sprecher des UN-Generalsekretärs Stéphane Dujarric in New York
Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane DujarricPicha: Imago/ZUMA Press/M. Brochstein

Lakini Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric aliyekuwa akitoa taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres huko New York, alizitaka pande zote mbili zilizo kwenye mzozo huo kusitisha mapigano zaidi.

"Anaitaka serikali ya Iraq na serikali ya kikanda ya Wakurdi, kuchukua hatua mwafaka kuzuia mapigano zaidi na kuenea kwa uvunjwaji wa sheria," alisema Dujarric. "Katibu Mkuu anazitaka pande zote husika kudhibiti hali hiyo kwa pamoja na kusuluhisha tofauti zote zilizoko kupitia mazungumzo, katika njia ambayo ni sambamba na katiba ya Iraq," aliongeza msemaji huyo.

Huku kikosi cha Iraq kikiwa kimechukua pia umiliki wa mji wa Sinjar kutoka kwa kikosi cha peshmerga, kikosi cha serikali hiyo ya kikanda kimeiteka afisi ya gavana na kambi muhimu za kijeshi na visima vya mafuta mjini Kirkuk.

Wasunni wenye itikadi kali wanawachukia Wayazidi

Sinjar ni eneo ambalo kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS, limefanya baadhi ya visa vibaya zaidi vya mauaji, ambapo maelfu ya wanaume wa Kiyazidi waliuwawa na maelfu ya wanawake na wasichana kutekwa nyara na kufanywa kuwa watumwa wa kingono mwaka 2014.

Jesdidin Jeside Frau Mutter mit Baby Flucht vor IS
Mwanamke wa Kiyazidi akiwa amembeba mwanawePicha: Getty Images/AFP/S.Hamed

Maelfu ya raia walikimbilia katika milima iliyo katika eneo hilo wakiwa katika hali mbaya mno, jambo lililoifanya Marekani kuingilia kati na kuanza kupambana na magaidi hao.

Wayazidi wanazungumza lugha ya Kikurdi lakini wanafuata imani yao wenyewe ambayo siyo ya Kiislamu na ni suala hilo ndilo lililowafanya Waislamu Wakisunni walio na itikadi kali kuwachukia.

Kufuatia hatua hiyo ya mwaka 2014 ambapo Wayazidi wengi waliyahama makaazi yao, walijitolea kupigana dhidi ya kundi linalojiita la IS, wakiwa katika makundi yao wenyewe ya waasi au yale yanayofadhiliwa na Wakurdi au serikali.

Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/Reuters/APE

Mhariri: Gakuba Daniel