1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanatuhumiwa kwa ubakaji

Sylvia Mwehozi18 Mei 2016

Umoja wa wa Mataifa umesema kuwa umepokea madai 44 ya unyanyasaji wa kingono uliofanywa na askari wake wa kulinda amani pamoja na baadhi ya wafanyakazi wake katika operesheni za kulinda amani katika nchi tofauti

https://p.dw.com/p/1IpjJ
UN-Soldaten in Mali
Picha: picture-alliance/dpa/T. Bindra

Umoja wa wa Mataifa umesema kuwa umepokea madai 44 ya unyanyasaji wa kingono uliofanywa na askari wake wa kulinda amani pamoja na baadhi ya wafanyakazi wake katika operesheni za kulinda amani katika nchi tofauti.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric amesema madai 29 yameripotiwa kufanywa na askari wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, 7 yakiripotiwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya na madai 2 nchini Haiti.

Nchi zingine ambako askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa wanatuhumiwa kufanya unyanyasaji wa kingono ni Sudan Kusini, Ivory Coast, Mali pamoja na eneo la mpakani la Abeyi baina ya Sudan na Sudan Kusini.

Askari wa kulinda amani walioko Libya na Mashariki ya kati nao pia wamekumbwa na kashfa hiyo.

Umoja wa Mataifa katika siku za hivi karibuni umekuwa katika tuhuma nzito za askari wake kutekeleza vitendo vya ubakaji kwa watoto na unyanyasaji wa kingono hasa katika nchi ya Afrika ya Kati na Kongo. Madai kama hayo pia yameripotiwa kufanywa na askari wa kulinda amani wa Ufaransa wanaojulikana kwa jina la Sangaris ambao wanaendesha harakati zao peke yao nchini Afrika ya Kati.

Mwanamke mjini Bangui akimpiga picha Askari wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani
Mwanamke mjini Bangui akimpiga picha Askari wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amaniPicha: Reuters/S. Rellandini

Ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwezi Machi ilisema kwamba jumla ya wanawake na wasichana 108 waliwasilisha madai yao ya kunyanyaswa kingono na askari hao katika eneo la Kemo nchini Afrika ya Kati kati ya mwaka 2013 hadi 2015.

Kundi moja la utetezi wa masuala ya maambukizi ya virusi vya UKIMWI lenye makao yake nchini Marekani AIDS-Free World ambalo lilikuwa la kwanza kutoa ripoti ya madai hayo , limesema kuwa hadi kufikia mwezi Aprili madai hayo yalifikia 41. Dujarric amesema hakuna taarifa mpya za uchunguzi kutoka Ofisi ya Uangalizi wa huduma za ndani kutoka Umoja wa Mataifa.

Umoja wa Mataifa una jumla ya askari 105,000 wa kulinda amani katika maeneo 16 yenye mizozo na idadi hiyo pia inajumuisha wale waliopo katika ujumbe wa kisiasa katika nchi za Afghanistan, Iraq na Somalia.

Kati ya madai yaliyowasilishwa mwaka huu, 35 yanawahusisha askari wa Umoja huo 11 kutoka Kongo, 6 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, 3 kutoka nchini Morocco, 3 Afrika ya Kusini na 4 ni askari wa Umoja wa Mataifa.

Wito wa kufanyiwa kazi tuhuma hizo

Jane Holl Lute aliteuliwa mwezi Februari kuwa mratibu wa Umoja wa Mataifa wa kushughulikia madai ya unyanyasaji kingono unaofanywa na askari wake,amesema hatua hiyo ilikuja baada ya kuonekana tatizo hilo halishughulikiwi ipasavyo.

Lute sasa anasema Umoja wa Mataifa unapaswa kushughulikia kile alichokiita "ajenda ngumu" ya ubakaji na unyanyasaji wa kingono hususan uliokithiri Afrika ya Kati.

Askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa
Askari wa kulinda amani wa Umoja wa MataifaPicha: dapd

"Inashangaza" anasema Lute katika mahojiano aliyoyafanya na shirika la habari la AFP. Mratibu huyo amesafiri hadi katika nchi zilizotajwa ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Afrika ya Kati. "Tunahitaji kutengeneza mazingira yasiyovumilia matendo hayo". Ziara yake mjini Bangui na Kinshasa ilimpa taswira halisi ya tuhuma hizo ambazo zinaonekana kuzidi katika nchi hizo mbili.

Uchunguzi wa madai matatu umekamilika.

Askari wa kulinda amani kutoka Bangladesh ambaye amehudumu nchini Afrika ya Kati amehukumiwa mwaka mmoja jela , kwa kosa la unyanyasaji wa kingono.

Mwingine anayetokea Misri akihudumu Afrika ya Kati naye amehukumiwa miaka 5 jela . Mfanyakazi mmoja wa Umoja wa Mataifa naye amesimamishwa kazi wakati uchunguzi ukiendelea. Taarifa hizi ni kwa mujibu wa msemaji wa Umoja huo.

Katibu mkuu Ban Ki-Moon amependekeza kwamba askari hao wanaotuhimiwa washitakiwe katika nchi ambako unyanyasaji huo umefanyika na Afrika ya Kusini ambayo imeonekana kukubaliana na uamuzi huo, imesema itamshitaki askari wake anayehudumu nchini Kongo. "Uamuzi huu utairuhusu jamii ya waathirika na wahanga nchini Kongo kuona kuwa haki imetendeka" anasema Dujarric.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi /AP/AFP

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman