Wanajeshi saba wa MONUSCO wanaolinda amani DRC wameuawa
16 Novemba 2018Majeshi ya DRC na yale ya Umoja wa mataifa Monusco, yanapigana bega kwa bega ili kulitokomeza kundi la waasi wa ADF kutoka Uganda katika viunga vya mji wa Beni hasa eneo la Mayangose katika mbuga la wanyama la Virunga.
Katika mapigano ya jana, askari saba wa Umoja wa Mataifa walipoteza Maisha na wengine kujeruhiwa.
Mapigano yameshuhudiwa katika viunga vya mji wa Beni, ambako majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo yakiungwa mkono na yale ya Umoja wa Mataifa, hasa kikosi chake maalumu cha kuingilia kati FIB yanapambana na waasi wa Uganda ADF katika mbuga ya wanyama ya Virunga Mayangose.
Wakati majeshi ya muungano yanashambulia ngome kadhaa za waasi wa ADF katika mbuga hiyo waasi hao waliunyemelea mji mdogo wa Oicha, ulioko umbali wa kilomita thelathini kaskazini mwa mji wa Beni jana Usiku, nakuwauwa raia watano, kuwajeruhi watu watatu,kupora maduka, pamoja na kuchoma moto nyumba kumi na mbili.
Shambulio la jana limeyasababisha mashirika ya kiraia mjini Beni kupitia mwenyekiti wake Kizito Bin Hangi, kutoa mwito kwa majeshi ya muungano, yaani jeshi la Congo na lile la Umoja wa mataifa Monusco, kuhakikisha kuwa yanawasambaza wanajeshi katika maeneo muhimu, ili kuwazuia waasi wa ADF kulipiza kisasi kwa raia kutoka na kipigo wanachokipata.
Mauwaji ya kila mara yanayofanywa na waasi wa ADF katika mji na wilaya ya Beni, yamesababisha familia kutawanyika. Operesheni zilizoanza jumatano iliyopita, zinaoneka kuboresha uhusiano baina ya jeshi na mashirika ya kiraia,na kwa hiyo, Kizito Bin Hangi anatoa mwito huu kwa raia ilikuunga mkono majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Monusco katika operesheni zinazodhaniwa kuwa,hatimae zitawaangamiza waasi wa ADF katika eneo hili.
Katika mapambano ya jana, wanajeshi saba wa Umoja wa mataifa walipoteza maisha yao, na wengine kujeruhiwa.
Umoja wa mataifa unasema kuwa wanajeshi wengi wa Congo waliuawa na wengine kujeruhiwa,bila ya kutaja idadi kamili ya waliouwawa.
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman