1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanajeshi 150 watorokea Eritrea kutoka Ethiopia.

Ramadhan ali10 Agosti 2006

Mvutano kati ya majirani wawili wa Pembe ya Afrika-Ethiopia na Eritrea unachukua sura mpya baada ya wanajeshi 150 wa ethiopia kutorokea Eritrea.Nchi hizi mbili zina ugomvi wa mpaka na zote 2 zimejiingiza katika mzozo wa sasa wa Somalia.

https://p.dw.com/p/CBIc

Kufuatia kutorokea Eritrea kwa brigedia-jamadari Kemal Gelchu wa Ethiopia,zaidi ya wanajeshi 150 wa Ethiopia, walivuka mpaka juzi jumaane na kukimbilia nao nchi jirani ya Eritrea.Hii imepalilia zaidi uhasama kati ya nchi hizi mbili zilizokwenda vitani juu ya ugomvi wa mpaka.

Zaidi ya wanajeshi 150 wa Ethiopia wametorokea Eritrea wakimfuata jamadari Kemal Gelchu.

Hii ni kwa muujibu vile maafisa walivyoripoti leo mjini Addis Ababa.Askari hao waliwasili Eritrea jumaane alfajiri ikiwa bado ni kiza kwa muujibu wa afisa wa kikosi cha kuhifadhi amani cha Umoja wa Mataifa.Afisa huyo wa UM amenukuliwa kusema,

“hatujui sababu za kutoroka kwa wanajeshi hao ,lakini yadhihirika, huu ni mkumbo wa kwanza mkubwa wa wanajeshi wa Ethiopia tuliowahi kuuona.”-mwisho wa kumnukulu.

Ethiopia, ilitangaza kutorokea Eritrea kwa Brig.

jenerali Geltu,aliekuwa kamanda wa kikosi cha 18 cha Jeshi la Ethiopia katika TV ya serikali,lakini haikuarifu kwamba wanajeshi wengine pia walimfuata huko.

Wakuu wa Jeshi la Ethiopia,hawakupatikana haraka kutoa maoni yao .

Eritrea imeeleza kwamba, jamadari Geltchu alivuka mpaka akifuatana na darzeni kadhaa ya maafisa wa hadhi ya juu jeshini,askari kadhaa pamoja na zana za kijeshi.

Hakuna thibitisho la taarifa hizo ,kwavile ethiopia iliarifu tu kuwa jamadari Geltchu ametoroka nchini.

Eritrea iliojinyakulia uhuru wake kutoka Ethiopia,1991,imearifu zaidi kuwa, jamadari Kemal Getchu alivuka mpaka katika mji mdogo wa mpakani wa Badme.

Mji huu,utakumbuka, ndio uliokua medani ya vita vikali baina ya nchi hizi mbili vya kuania mpaka vilivyochukua maisha ya watu 70.000 na kumalizika kwa mapatano ya amani ya mwaka 2000.Chini ya mapatano hayo,pande zote mbili zilikubali kuridhia hukumu ya mahkama huru juu ya ugomvi wao wa mpakani.

Wizara ya habari ya Eritrea lakini, imetoa taarifa ikithibitisha kutoroka huko kwa wanajeshi hao na ikitoa sababu za machafuko yaliozuka mwaka jana huko Ethiopia kutokana na matokeo ya uchaguzi ya kutatanisha yaliokirejesha chama tawala madarakani kwa kipindi kingine cha miaka 5.

Vyombo vya habari vya serikali za nchi zote mbili-Ethiopia na Eritrea, vina tabia ya mara kwa mara kuripoti kutoroka kwa wanajeshi wa kila upande kwa mwenziwe,lakini, kutoroka kwa Brig.Jenerali Kemal Gelchu, ndiko afisa wa hadhi ya juu kabisa hadi sasa.

Isitoshe, tokeo hili limezuka huku mvutano ukiwepo kati ya majirani hawa 2 wa Pembe ya Afrika juu ya matatizo ambayo hayakupatiwa bado ufumbuzi kuhusiana na vita vyao vya mpakani kati ya 1998-2000 pamoja na msukosuko unaoendelea sasa katika nchi jirani ya Somalia.

Katika mzozo huo, Ethiopia inaiungamkono serikali ya mpito ya Somalia yenye maskani yake mjini Baidoa wakati Eritrea inaungamkono ule utawala wa kiislamu wa mahkama za kisharia mjini Mogadishu.

Mpaka kati ya nchi hizo mbili unalindwa vikali na kila upande na unakaguliwa na kikosi cha UM mpaka kati ya nchi hizo mbili,kumeikera mno Asmara inayoshikilia hukumu iliokatwa na Mahkama huru iheshimiwe na Addis Ababa.