Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu Kenya watuzwa
27 Novemba 2020Kadhalika serikali imehimizwa kuwezesha mazingira salama na sera zitakazohakikisha wanaharakati wamelindwa na haki za kibinadamu zimezingatiwa kwa kila mmoja.
Wanaharakati nchini wanatekeleza majukumu yao katika mazingira ambayo kwa wakati mwingine yamekuwa tishio kwa maisha yao. Mwanamme mmoja wa makamo kutoka eneo la bonde la ufa ambaye hakutaka kutajwa jina kwa misingi ya kiusalama, alisimulia jinsi alivyonusurika kifo katika kipindi cha baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 na uchaguzi wa mwaka 2017, hata kumlazimu kukimbilia usalama wake nje ya nchi.
Alikuwa mmoja wa wanaharakati nchini Kenya waliokuwa wakizitetea baadhi ya jamii zilizoathiriwa na ghasia za baada ya uchaguzi, waliowapoteza wapendwa wao na mali kufuatia ghasia hizo eneo la bonde la ufa.
Chake ni kisa kimoja kati ya mengi yanayowasibu wanaharakati nchini Kenya. Kadhalika, kipindi hiki ambapo serikali iliidhinisha masharti ya kupambana na ueneaji wa ugonjwa wa COVID 19, matukio mengi ya ukiukaji wa haki za kibinadamu yameripotiwa yakiwemo dhuluma za kijinsia, za kingono na dhuluma katika mikono ya maafisa wa polisi.
Baadhi ya jamii vilevile waliuchukua muda huu kuendeleza tamaduni zilizopitwa na wakati kama vile ukeketaji na ndoa za mapema. Wanaharakati wanaitaka serikali kuwapa mazingira mazuri ya kufanyia kazi na kuchunguza mashambulizi dhidi yao.
Elizabeth Kipsang ambaye ni mwakilishi wa bunge la Baringo ambaye amekuwa kwenye mstari wa mbele kutetea haki za binadamu, amesema ipo haja ya kuweka sera zinazohakikisha haki za kila mmoja zinazingatiwa
Wanaharakati hao wamenukuu takwimu na matukio ya ukiukaji wa haki za kibinadamu nchini, kama nia mojawapo ya kuhimiza uzingatiaji wa sheria za kikatiba na makubaliano ya kimataifa kuhusu haki za kibinadamu.