1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati Tanzania wataka katiba mpya

29 Juni 2021

Wanaharakati wanaopigania katiba mpya na haki za kisiasa nchini Tanzania, wamemtaka Rais Samia Suluhu Hassan akamilishe mchakato huo ambao ulikuwa umebakiza hatua chache.

https://p.dw.com/p/3vkKo
Uganda Unterschrift EACOP in Kampala
Picha: Presidential Press Unit/Uganda

Kauli hiyo wameitoa baada ya Rais Samia kuomba apewe muda kwanza ili aimarishe uchumi ambao amesema umeyumba kabla ya kurejesha mezani suala la katiba mpya.

Akizungumzwa na watendaji wandamizi wa vyombo vya habari vya ndani na kimataifa katika ikulu ya Dar es Salaam siku ya Jumatatu, Rais Samia aliashiria kuliweka kando suala la katiba mpya pamoja na haki ya vyama vya kisiasa kuandaa mikutano ya hadhara kama inavyoainisha katiba ya sasa, akisema siyo kwamba katiba si ya maana, bali anahitaji muda kuujenga uchumi kwanza.

Jambo hilo litaharibu sifa yake

Wanaharakati hao wamesema hatua ya rais kulipiga danadana suala la katiba itamuharibia sifa aliyojijengea miongoni mwa wananchi walioonesha matumaini makubwa kwake.

Soma zaidi: Kiongozi wa upinzani Tanzania ataka katiba mpya

Onesmo Ole Ngurumo, mratibu wa mtandao wa haki za binadamu nchini Tanzania, amekumbusha kuwa suala la katiba ni suala la Watanzania na kwamba taifa tayari limeshatumia rasilimali nyingi kuandaa katiba ambayo wenyewe waliitaka na kuonya kuwa ni kosa kubwa kudhani kwamba mtu mmoja anaweza kuamua lini katiba inaweza kupatikana.

Tansania Pressekonferenz zu Übegriffen auf Journalisten
Onesmo Ole Ngurumo (Kushoto), Mratibu wa Mtandao wa Haki za Binadamu Tanzania, THDRC Picha: DW/S. Khamis

Kwa upande wake, mkurugenzi wa habari na uenezi wa chama cha Wananchi CUF Mohamed Ngulangwa, amesema kwa sasa hakuna kipaumbele kinachostahili kuzingatiwa katika utawala wa Rais Samia kabla ya katiba mpya, kutokana na yale yaliyotokea katika utawala wa mtangulizi wake.

Aidha, wamesema pia kwa kuzingatia uhalisia kwamba katiba ya sasa ilishaonekana kuwa haiendani na mazingira ya sasa, hali iliyosababisha kuandaa mchakato wa kutafuata katiba mpya mnamo mwaka wa 2010.

Rais apewe muda

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, kuna haja ya kumpa nafasi ili akamilishe yale ambayo ameyawekea kipaumbele, kwani katika kipindi cha siku 100 madarakani ameweza kufanya mengi makubwa ambayo yalitazamwa kama ni ukiukaji wa haki za raia, demokrasia na hata uchumi kwenda kombo.

Mchambuzi wa siasa na diplomasia Saidi Msonga, amesema kila kitu hakiwezi kufanyika kwa usiku mmoja, hivyo rais apewe muda.

Rais Samia amekuwa akikutana na makundi mbalimbali katika jamii nchini kuainisha vipaumbele vya serikali yake na pia kusikiliza maoni ya makundi hayo, ambapo mpaka sasa amekutana na kuzungumza na wazee, viongozi wa dini, wanawake, wafanyabiashara, vijana na watendaji wa sekta ya habari, huku akitimiza masuala kadhaa yaliogusa nyoyo za Watanzania.