1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati: Mabadiliko ya tabianchi ni lazima

15 Novemba 2024

Wanaharakati wa mabadiliko ya tabianchi wanasema Ujerumani lazima iongoze katika harakati za mabadiliko ya tabia nchi katika Mkutano wa COP29 unaoendelea mjini Baku, licha ya migogoro ya ndani inayoikabili serikali yake.

https://p.dw.com/p/4n3Wm
Azerbaijan -COP29
Bango la mwanaharakati wa mazingira lenye maneno ya kupinga kuendelea kwa matumizi ya nishati ya mafuta.Picha: Aziz Karimov/REUTERS

Suala la msingi katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi ni jinsi gani nchi zilizoendelea kiviwanda zitasaidia nchi maskini katika siku zijazo na uwekezaji katika ulinzi wa hali ya hewa na kukabiliana na athari zake, lakini pia katika kuondokana na uharibifu.

Soma pia: Mkutano wa COP29 waghubikwa na joto la kidiplomasia

Akizungumza katika mkutano huo mwanaharakati wa kundi la mazingira la Fridays for Future, Luisa Neubauer, amesema wanatarajia kwamba Ujerumani na Umoja wa Ulaya watatimiza wajibu wao.

Hata hivyo, utata unaibuka katika kubaini kiasi cha fedha kinachopaswa kulipwa na walipa kodi. Ujerumani imesisitiza mara kwa mara kwamba inatumai uwekezaji mkubwa zaidi utatoka katika uwekezaji wa kibinafsi.

Waziri wa mazingira wa Ujerumani, Jennifer Morgan, amesema, suala la kiasi cha fedha ambacho Ujerumani inaweza kukitumia katika siku zijazo litategemeana na uamuzi wa serikali. Uchaguzi unatarajiwa mnamo Februari 23, baada ya muungano tawala wa Kansela Olaf Scholz kuanguka wiki iliyopita.

Changamoto katika kufikia malengo

Azerbaijan -Baku COP29
Mkuu wa sera ya mabadiliko ya tabianchi wa Umoja wa Mataifa, Simon Stiell, akitoa hutoba wakati wa mkutano wa COP29 mjini Baku.Picha: Alexander Nemenov/AFP

Kongamano hilo mwaka huu lilitakiwa kujikita zaidi kwenye ajenda ya hali ya sayari ya dunia, badala yake unagubikwa na siasa za kijiografia zenye misukosuko, kauli kali za makabiliano pamoja na kuchaguliwa tena kwa mkosoaji wa masuala ya athari za mabadiliko ya tabianchi, Donald Trump wa Marekani.

Soma pia: Tofauti zaibuka katika mkutano wa COP29

Waziri wa nishati wa Marekani, Jennifer M. Granholm, amesema mabadiliko kutoka nishati ya mafuta kwenda kwenye nishati zilizo salama kwa mazingira "yanafanyika ulimwenguni" na kwamba nchi hazirudi nyuma:

"Kwa hiyo ujumbe wetu ni kwamba bila kujali nani anaingia Ikulu, mabadiliko haya yanafanyika. Yanafanyika Marekani katika ngazi ya chini na sekta binafsi na mashirika yasiyo ya kiserikali. Inatokea duniani kote na nchi ambazo nyinyi munawakilisha hakuna kurudi nyuma."

"Kutokuwepo kwa uongozi katika Ikulu ya Marekani hakumaanishi kuwa mpito huu wa nishati umesitishwa. Ningesema kinyume chake, huu ni wakati wa kuongeza kasi ya kujaza pengo ambalo linaweza kuachwa na uongozi nchini Marekani."

Granholm ameongeza kusema kwamba mustakabali wa sera ya tabianchi nchini Marekani hautabiriki, akikumbushia uamuzi wa Trump wakati wa muhula wake wa kwanza madarakani kujiondoa kwenye Mkataba wa Paris.