1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanahabari Tanzania watakiwa kutahadhari dhidi ya corona

15 Aprili 2020

Waandishi wa habari nchini Tanzania wametakiwa kuchukua tahadhari wakati wakitimiza majukumu yao hasa wakati huu wa mlipuko wa COVID-19, huku tayari nchi hiyo ikiwa imethibitisha watu 53 kukumbwa na maambukizi hayo.

https://p.dw.com/p/3avqh
Tansania Interview DW-Reporterin Salma Said
Picha: DW

Mkusanyiko wa mashirika matatu, baraza la habari nchini(MCT) Jukwaa la Wahariri na mtandao wa watetezi wa haki za binadamu yametoa mwongozo ukiwalenga waandishi wa habari kuhusiana na hatua wanazopaswa kuchukua wakati wakiwa kwenye kazi zao.

Hayo yanajitokeza huku idadi ya waandishi wa habari waliokumbwa na janga hilo wakifikia wawili, mmoja akiwa mwakilishi wa DW Visiwani Zanzibar na miwngine kutoka shirika la utangazaji la taifa.

Akibainisha kuhusu mwongozo huo, Mwenyekiti wa jukwaa la wahariri, Deudatus Balile amesema wakati huu ni wa hatari zaidi kwa wanahabari kutokana na mazingira ya kazi zao ambazo wakati mwngine zinawalazimu kujitumbukiza kwenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

Wakati wanahabari wakiendelea kutolewa rai namna wanavyopaswa kuwa makini katika utendaji wao wa kazi, idadi ya watu wanakumbwa na maambukizi ya virusi vya corona imeendelea kuongezeka na hadi ripoti hii inakwenda hewani tayari watu 53 walikuwa wamethibitishwa.

Waandishi wa habari watakiwa kujikinga dhidi ya corona wanapofanya kazi zao
Waandishi wa habari watakiwa kujikinga dhidi ya corona wanapofanya kazi zaoPicha: Picture-alliance/AA/Z. H. Chowdhury

Waziri Mkuu Kassim Majaiwa ambaye jana alitangaza  shule na vyuo kuendelea kufungwa kwa muda usiojulikana, amewatolewa mwito wananchi kuchukua tahadhari zaidi akiwataka kujiepusha na misongamano.

Katika hatua nyingine, wakuu wa jumuiya ya afrika mashairki wamepanga kufanya mkutano wa dharura kwa ajili ya kujadili tishio la corona linaloendelea kuisumbua dunia.

Mkutano huo ambao unafanyika kwa njia ya vidio hajaelezwa lini utafanyika lakini katika mtandao wake wa Twiter, sekretariati ya jumuiya hiyo imesema kikao hicho hicho kitawahusisha viongozi wote wan chi wanachama wa jumuiya hiyo.

Mbali ya kujadili tishio hilo la Corona, wakuu hao watajikita pia katika kuangalia maambukizi ya Covid-19 hayaathiri biashara ndani ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo yenye nchi wanachama sita.

Hayo yanakuja katika wakati ambapo ripoti ya Benki ya Dunia ikionya kuwa sekta ya utalii ndio itaathirika zaidi katika jumuiya ya Afrika mashariki kutokana na athari za kusambaa kwa Corona.

Mwandishi: George Njogopa/DW Dar es Salaam