1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiNigeria

Karibu wanafunzi 20 wa vyuo vikuu nchini Nigeria watekwa

17 Agosti 2024

Karibu wanafunzi 20 wa chuo kikuu cha Nigeria wametekwa na watu wenye silaha waliovizia magari yao kaskazini mwa nchi hiyo.

https://p.dw.com/p/4jZUK
Nigeria inakabiliwa na matukio ya utekaji wa wanafunzi na watekaji kudai kikomboleo
Karibu wanafunzi 20 wa vyuo vikuu nchini Nigeria ikiwa ni pamoja na cha Maiduguri wametekwa na watu wenye silaha

Msemaji wa jeshi la polisi katika eneo la Benue Catherine Anene amesema jana kwamba wanafunzi hao walikuwa wakielekea kusini mwa nchi kushiriki mkutano wa wanafunzi wanaosomea udaktari wakati walipovamiwa katika jimbo la Benue Alhamisi jioni.

Amesema shambulizi hilo lilitokea kando ya barabara ya Benue's Otukpo, mahali palipojulikana sana kwa utekaji nyara.

Wanafunzi waliotekwa ni wa vyuo vikuu vya Maiduguri na Jos, vyote vya kaskazini mwa Nigeria na tayari wanafunzi wenzao wamelaani tukio hilo na kuzitaka mamlaka kuwalinda wanafunzi na kuhakikisha wenzao wanaachiliwa.

Haikubainika mara moja ni kundi gani lililofanya shambulizi hilo au mahali ambapo mateka walipelekwa na polisi bado ilikuwa haijasema chochote kuhusiana na juhudi za kuwaokoa.

Kiongozi wa wanafunzi wa chuo kikuu cha Maiduguri Ijaban Bajam amesema kwenye taarifa yake kwamba wamesikitishwa na kitendo hicho na kutoa wito wa wanafunzi hao kurudi salama.