1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanadiplomasia wakutana Vienna kuujadili mzozo wa Syria

23 Oktoba 2015

Wanadiplomasia wa ngazi ya juu kutoka Urusi, Marekani, Saudi Arabia na Uturuki watafanya mazungumzo leo kuhusu vita vya Syria baada ya Urusi kujihusisha katika kampeini ya kijeshi Syria kumsaidia Rais Bashar al Assad.

https://p.dw.com/p/1GszC
Picha: picture-alliance/dpa/Ministry of Foreign Affairs of the Russian Federation

Mawaziri wa mambo ya nje wa Marekani, Saudi Arabia na Uturuki ambao nchi zao zinayaunga mkono makundi ya waasi wanaotaka kumng'oa madarakani Rais Bashar Al Assad nchini Syria, wanalenga kufanya mazungumzo na mwenzao wa Urusi Sergei Lavrov mjini Vienna, Austria baada ya Rais wa Syria kufanya ziara ya kushutukiza mjini Washington wiki hii kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Mnamo tarehe 30 mwezi Septemba, Urusi ilianzisha mashambulizi ya angani nchini Syria dhidi ya wanamgambo wenye itikadi kali wa kundi la dola la kiislamu IS ambao wanayadhibiti maeneo makubwa nchini humo na kuutishia utawala wa Assad ambaye ni mshirika mkubwa wa Urusi.

Urusi yabadilisha mkondo wa vita vya Syria

Kujihusisha kwa Urusi katika vita hivyo vya Syria ambavyo vimedumu kwa takriban miaka minne unusu sasa, kwa kuwapiga jeki wanajeshi wa serikali ya Syria, kumebadilisha mkondo wa kampeini ya kijeshi ya mashambulizi ya angani yanayoongozwa na Marekani na washirika wake nchini humo dhidi ya IS.

Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov na wa Marekani John Kerry
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov na wa Marekani John KerryPicha: picture-alliance/AP Photo

Marekani na nchi washirika wa kanda hiyo wameyashutumu mashambulizi hayo yanayofanywa na Urusi na kudai hayawalengi hasa wanamgambo wa IS bali makundi ya waasi wanaompinga Assad na kuhoji kujiingiza kwa Urusi katika mzozo huo kutasababisha kuendelea kwa vita hivyo vya Syria kwa muda mrefu zaidi.

Kabla ya mkutano huo wa leo, hatma ya Assad kisiasa bado inasalia kuwa suala tete kati ya Urusi na nchi hizo nyingine tatu baada ya miaka minne ya kushindwa kukomesha umwagaji wa damu nchini humo huku kukiwa na matumaini finyu kuwa ufumbuzi wa mzozo huo utapatikana hivi karibuni.

Marekani na washirika wake zimekuwa zikisisitiza sharti Assad ang'atuke madarakani ndipo kuwe na suluhisho la kisiasa katika vita hivyo ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 250,000 na kusababisha mamilioni ya wengine kuachwa bila ya makaazi na kuwa wakimbizi.

Urusi kwa upande wake imeshikilia kuwa lazima kwanza imsaidie Assad kupambana dhidi ya wanamgambo wa IS na makundi mengine ya kigaidi kabla ya kuanza kwa mazungumzo kuhusu mageuzi ya utawala.

Hapo jana akiwa mjini Sochi, Putin alisema dhamira ya Marekani ni kumng'oa Assad madarakani lakini lengo lao Urusi ni kuushinda ugaidi ili kuwe na mazingira muafaka ya kuanzishwa mchakato wa kutafuta suluhisho la kisiasa na kufikia makubaliano ya kudumu.

Assad aondoke au asiondoke?

Akiwa mjini Berlin, naye Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema huku pande zote zikikubaliana kuhusu haja ya kupatikana kwa suluhisho la kisiasa kwa mzozo wa Syria na kupambana dhidi ya IS kitu kimoja ndicho kikwazo kikubwa nacho ni mtu aitwaye Bashar al Assad.

Rais wa Syria wa Bashar al Assad na Rais wa Urusi Vladimir Putin
Rais wa Syria wa Bashar al Assad na Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/RIA Novosti/Kremlin/A. Druzhinin

Iran ambayo pia ni mshirika wa karibu wa utawala wa Assad na mojawapo ya nchi zenye usemi katika kanda hiyo haijaalikwa katika mazungumzo hayo ya Vienna kwa sababu ya pingamizi kutoka kwa Saudi Arabia.

Mbali na suala hilo la mzozo wa Syria, Kerry na Lavrov watafanya mazungumzo na wawakilishi wa Umoja wa Ulaya na wa Umoja wa Mataifa kuhusu mzozo kati ya Israel na Palestina.

Mwandishi: Caro Robi/afp

Mhariri: Josephat Charo