1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanachokitaka vijana wa Tanazania uchaguzi 2015

Elizabeth Shoo18 Oktoba 2015

Vijana ndio wanaounda kundi kubwa la watu Tanzania na wana nguvu kubwa ya kuamua uchaguzi. Baadhi yao wanaelezea wanavyoshiriki kwenye shughuli za kisiasa na wanachokitarajia kutoka kwa serikali.

https://p.dw.com/p/1Gq4N
Vijana Tanzania
Picha: picture-alliance/AFP/D. Hayduk

Mara tatu kwa wiki, Gladness Machange anakwenda kazini. Anatunza mazingira ya nyumba ya familia moja mjini Moshi, Tanzania. Yeye ni mmoja wa wananchi milioni 23 waliojiandikisha kupiga kura. Na kama Watanzania wengine, Gladness anatamani kiongozi atakayeleta mabadiliko. Kwa mfano kupunguza ada za shule ili kila anayetaka kusoma aweze kusoma. Yeye hakuwa na bahati ya kumaliza kidato cha nne: "Ada ya kidato cha tatu na cha nne ililipiwa yote," anasema Gladness. "Nilipofika kidato cha nne ada ikashindikana. Baba akaniambia 'Kaa nyumbani, mimi sina hela'" Anasema kama angeweza kuendelea na masomo yake, leo asingekuwa anatilia maji maua na kufagia uwanja nyumbani kwa watu. "Ungekuta sasa hivi nimekuwa mwalimu au niko chuo."

Vijana wanaunda karibu asilimia 40 ya idadi ya raia wa Tanzania. Wana nguvu kubwa ya maamuzi na ya kubadilisha nchi. Kura yao ina uzito. Ndio maana kwenye mikutano mingi ya kampeni, wagombea madaraka wamekuwa wakitoa ahadi kwa vijana.

Suala ambalo vijana wengi wametaja kuwa linawahusu, ni ajira. Kuna ahadi kwamba nafasi za kazi kwa vijana zitatengenezwa hasa kwenye sekta ya viwanda. Hata hivyo, Nchang'wa Nhumba ambaye ni mwanafunzi wa udaktari, chuo kikuu cha KCMC Moshi, ana mashaka. "Vijana sasa hivi wamechoshwa na ahadi zisizotimizika. Kila mwaka wanakuja na maneno matamu. Serikali inayokuja inatakiwa ijitahidi kutimiza angalau asilimia 85 ya ahadi zote." Nchang'wa anaamini hapo kiu ya vijana itatulizwa.

Vijana wakiuza na kununua mitumba jijini Dar es Salaam
Vijana wakiuza na kununua mitumba jijini Dar es SalaamPicha: DW/K. Kaminski

Vizuizi kwa wanafunzi

Wakati vijana wengi sasa wameonyesha moyo wa kushiriki katika zoezi la kupiga kura ili kuamua mustakabali wa nchi, wapo baadhi waliokosa nafasi hiyo. Huyu hapa pia ni mwanafunzi wa chuo cha KCMC: "Tulitakiwa tujiandikishe tukiwa bado masomoni. Kulikuwa na watu kama wanne wa kuandikisha zaidi ya watu 3,000 ndani ya siku tano na bado kuna kupiga picha, kutia saini na kutafuta vyeti. Kwa muda tuliopewa tusingeweza kumaliza wote."

Kulingana na taarifa za mwanafunzi huyo, walipoomba wapewe muda zaidi, wale waandikishaji walisema wao ni wajumbe tu, na kwamba suala hilo linatakiwa kushughulikiwa na Tume ya uchaguzi.

Baadhi ya wananchi wa Tanzania wameelezea wasiwasi wao kuhusu tetesi kwamba vyama vya siasa vinawahamasisha vijana kuleta vurugu wakati wa uchaguzi. Ili kuhakikisha amani inatawala, shirikisho la vyuo vya elimu ya juu nchini Tanzania limekuwa likifanya makongamano makubwa yanayolenga hasa wanafunzi wa vyuo ili kuhimiza utulivu.

Vijana wengi wamesema wanatamani serikali ijayo iyajali maslahi yao. Wakati huo huo, lawama zimetupwa kwa serikali iliyopita kwa kushindwa kuwatengenezea vijana maisha mazuri. Israel Augustine ni kijana anayefanya biashara mjini Shinyanga. Amehudhuria mikutano ya kampeni na ana mpango wa kuwa mwanasiasa baadaye. Amesema CCM haijafanya kosa lolote. "Vijana wengi wanasubiri kuwekewa hela mfukoni na serikali, kitu ambacho serikali yoyote duniani haiwezi kufanya. Serikali zinatengeneza mazingira ya vijana kufanya kazi." Israel anaongezea kuwa vijana wenyewe wakati mwingine wanapoishia kuwa walevi wanakuwa hawasaidiki tena.

Vyama vyote vimetoa ahadi kwa vijana
Vyama vyote vimetoa ahadi kwa vijanaPicha: DW/E. Shoo

Hata hivyo, yeye pia anaitaka serikali ijayo itoe ahadi zinazotimizika, sio ambazo zinatekelezeka ndani ya miaka 20, wakati kipindi cha uongozi ni miaka mitano tu.

Mwandishi: Elizabeth Shoo

Mhariri: Mohammed Dahman