1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanachama wa Shirika la OPEC kukutana kesho Vienna.

23 Oktoba 2008

Ni kupunguza kiwango cha utoaji mafuta kwa sababu ya kuanguka bei .

https://p.dw.com/p/FfWO
Rais wa Shirika la OPEC, waziri wa nishati na madini wa Algeria Chakib Khelil.Picha: AP

Mataifa yenye msimamo mkali , wanachama wa Shirika la nchi zinazotoa mafuta kwa wingi OPEC, leo wameimarisha shinikizo lao kuhusu takwa la kutaka kupunguzwe kiwango cha utoaji mafuta, wakati wa mkutano wao wa dharura mjini Vienna kesho.hayo yanatokea katika wakati ambao dunia inakabiliwa na kitisho cha hali mbaya ya uchumi.

Waziri wa mafuta wa Iran Gholam Hossein Nozari alisababisha mgawanyiko katika shirika hilo, juu ya kuanguka bei ya mafuta, wakati alipotoa wito jana wakati alipowasili mjini Vienna wa kupunguzwa mapipa milioni mbili kwa siku. Akasema mapipa milioni mbili yataleta utulivu katika masoko.

Libya, Venezuela na Qatar nazo pia zimekua zikisisitiza mnamo siku za hivi kariuni juu ya kupunguzwa kiwango cha utoaji mafuta katika nchi wanachama wa OPEC.

Lakini viongozi wa nchi za magharibi kama Waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown wanapinga. Brown anasema kupunguzwa kokote kutakua ni " kashfa" na mataifa ya Ghuba yakiongozwa na Saudi Arabia yanatarajiwa kupinga hatua yoyote ya kupunguza viwango vya utoaji mafuta katika Shirika hilo.

Afisa mmoja wa OPEC hata hivyo alisema haiwajibiki kuendelea kutoa mafuta wakati bei ni za chini, kwa madhumuni tu ya kupunguza machungu katika nchi za magharibi, yaliosababishwa na msukosuko wa fedha ambao chanzo chake ni baadhi ya mabenki yao makubwa.

Pamoja na hayo wadadisi wanatarajia OPEC itafikia uamuzi wa kupunguza utoaji mafuta alau kwa kiwango cha mapipa milioni moja kwa siku.

Rais wa Shirika hilo Chakib Khelil, ambaye ni waziri awa nishati wa Algeria, alisema jana kwamba shirika la OPEC limeshaathirika kutokana na msukosuko wa fedha pamoja hatari ya kukumbwa na bei ya chini zaidi ya mafuta. Lakini akaongeza kwamba hawana budi kuhakikisha maamuzi yao ya kupunguza viwango vya utoaji mafuta yanaweka wizani na zingatio kwa wanunuzi na pia watoaji.

Shirika la OPEC hutoa asili mia 40 ya mafuta ya dunia na kiwango chake rasmi ni mapapipa 28 . 8 milioni kwa siku. Iran ni msafirishaji mafuta wa pili mkubwa kabisa katika Shirika hilo na uchumi wake hutegemea zaidi mapato yanayotokana na mafuta na gesi. Saudi arabia ndiyo msafirishaji mkubwa wa mafuta yasio safishwa duniani.

Urusi ndiyo mtoaji mkubwa kabisa wa mafuta miongoni mwa mataifa ayasio wachama wa OPEC . Akizungumza mjini Moscow Rais Dmitry Medvedev alimwambia katibu mkuu wa OPEC Abdullah Salem El Badri kuwa anataka ushirikiano wa karibu na Shirika hilo lenye wanachama 12.

Mkutano huo wa Vienna juu ya athari za sukosuko wa fedha duniani na kuanguka kwa bei katika soko la mafuta duniani, awali ulipangwa kufanyika tarehe 18 mwezi ujao wa Novemba, lakini umesogezwa mbele na kufanyika kesho kwa sababu ya kuanguka mno kwa bei ya mafuta.