Wanachama wa NATO wajadili kuongeza vikosi Afghanistan.
21 Septemba 2009Msemaji wa Jumuia ya Kujihami ya nchi za Nato James Appathurai amesema leo kwamba mabalozi kutoka nchi 29 za Jumuia ya Kujihami ya NATO wanaitathmini ripoti ya Afisa huyo wa Ngazi ya Juu wa Jeshi la Marekani Jenerali Stanley Mc Chrystal.
Sehemu ya majadiliano hayo yalivuja kwa Vyombo vya habari na kuchapishwa, ambapo gazeti la Washngton Post lilikuwa la kwanza kuiripoti jana jioni.
Kwenye waraka yenye kurasa 66, Jenerali huyo wa Kimarekani aliitaka NATO na mataifa washirika kuongezea nguvu majeshi hayo yanayopambana na Wapiganaji wa Taliban ili kuweza kuziba pengo mpaka pale Jeshi la Afghanistan litakapoimarika.
Aidha msemaji huyo wa NATO amekataa kuzungumzia yaliyomo katika ripoti hiyo na kusema kuwa ni mada ya majadiliano ya kawaida.
Amefahamisha kuwa katika siku zijazo watajadili pia mataifa yasiyo wanachama wa NATO, yaliyosehemu ya Jeshi la kulinda amani ISAF linaloongozwa na NATO.
Kwa mujibu wa wanadiplomasia wa nchi za NATO, kurasa ziliyoainishwa hazifafanui kwa kina idadi ya wanajeshi na vifaa ambavyo Jenerali McChrystal anadhani vinaweza kuhitajika kufanya kazi hiyo.
Wakati huohuo Maafisa wa polisi kutoka katika mikoa yenye machafuko mengi nchini Afghanistan wamehoji mahitaji ya kuongezwa kwa vikosi zaidi vya majeshi ya Marekani, kwa kusema kuwa hali hiyo itaongeza wao kujitambua kuwa wanatawaliwa na kwamba fungu la fedha kwa ajili ya shughuli hiyo lingepaswa kutumiwa kwa ajili ya vikosi vya nchi hiyo.
Kauli hiyo ya Maafisa hao wa polisi wa Afghanistan imekuja kufuatia ripoti hiyo ya Jenerali Stanley McChrystal, Afisa wa ngazi ya Juu ya Jeshi la Marekani na Kamanda wa NATO Afghanistan, ikionya kuwa vita hivyo vinazidi kuwa vibaya na kwamba majeshi hayo ya kigeni yanaweza kushindwa iwapo hakutaongezwa vikosi zaidi.
Hayo yote yanajitokeza katika wakati ambao nchini Italia kwa mfano wito wa kutaka majeshi ya nchi hiyo yaondolewe Afghanistan baada ya wanajeshi wake wengine kuuawa unaongezeka. Idadi ya wanajeshi wa Italia waliouwawa Afghanistan sasa imefikia 21.
Rais Barack Obama wa Marekani mapema mwaka huu aliidhinisha kupelekwa wanajeshi elfu 21 zaidi nchini Afghanista na kufanya jumla ya wanajeshi wa Marekani nchini humo kufikia elfu 68 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Mawandishi:Halima Nyanza /AFPE
Mahariri:M.Abdul-Rahman