1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanachama wa CDU wamchagua tena Merkel

3 Aprili 2017

Kansela Angela Merkel amechaguliwa tena kukiongoza chama chake cha kihafidhina cha Christian Democratic Union, CDU, na kugombea muhula wa nne madarakani, uchaguzi mkuu utakapoitishwa msimu wa mapukutiko mwakani.

https://p.dw.com/p/2Tpxz
Angela Merkel CDU Parteitag in Essen
Picha: DW/K.-A. Scholz

Katika hotuba yake iliyochukua sura ya ilani ya uchaguzi mkuu kansela Angela Merkel amezungumzia mada zote kuanzia kuzidi hisia za kizalendo nchini Ujerumani na kwengineko ulimwenguni,umuhimu wa kuhifadhiwa maadili ya kidemokrasia hasa baada ya kuchaguliwa Donald Trump kuwa rais wa Marekani, kura ya Brexit ya Uingereza mpaka kufikia kujiuzulu waziri mkuu wa Italy Matteo Renzi. Katika hotuba yake hiyo kansela Merkel ametahadharisha dhidi ya "ahadi zisizokuwa na msingi " zinazotolewa na makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia yanayojidai kuwa peke yao ndio wanaowakilisha wananchi.

Wakati huo huo ametilia mkazo msimamo wake na wa chama chake cha CDU katika kulinda maadili ya Ujerumani akielezea dhamiri  ya serikali yake kupiga marufuku watu kuvaa mavazi yanayomfunika kuanzia kichwani mpaka kidole gumba wanapokuwa katika baadhi ya vituo vya huduma za jamii. Amekumbusha sheria ya Ujerumani inabidi itangulizwe mbele.

 

Angela Merkel ahutubia mkutano mkuu wa CDU mjini Essen
Angela Merkel ahutubia mkutano mkuu wa CDU mjini EssenPicha: Getty Images/AFP/T. Schwarz

Wananchi ni sisi na sio baadhi ya wachache anasema Kansela

Katika hotuba hiyo ya saa moja, dakika 18 na sekondi 36 iliyokuwa kila wakati ikishangiriwa kwa kupigiwa makofi, kansela amekionya chama chake kwamba uchaguzi mkuu mwaka 2017 "utakuwa mkali kuwahi kushuhudiwa tangu Ujerumani zilipoungana upya mwaka 1990, kutokana na  kupata nguvu hisia za kizalendo, kupitia chama cha Chaguo Mbadala kwa Ujerumani AfD.

"Lakini dunia haina rangi nyeupe na nyeusi tu na tunabidi tuwe macho dhidi ya wenye kutoa majibu ya kijuu juu kwa sababu hayajawahi kuijongeza mbele nchi yetu" amesema kansela Merkel. Amewakosoa zaidi wale wanaopaza sauti wakidai "Wananchi ni wao",kauli mbiu iliyohanikiza wakati wa maandamano ya chama cha siasa kali za mrengo wa kulia Pegida, wakiigiza kauli ile ile iliyokuwa imehanikiza mwishoni mwa mwaka 1989 katika Ujerumani Mashariki ya zamani kudai ukome utawala wa kikoministi wakati ule.

"Wananchi kwa jumla ndio wanaoamua nani ni wananchi,sisi bado ndio tunaoamua na sio baadhi ya watu,hata kama wanapaza sauti", amesema Angela Merkel.

Akikosolewa mpaka katika chama chake cha CDU kutokana na sera zake za milango wazi zilizopelekea mwaka 2015 maelfu ya wakimbizi kuingia humu nchini,kansela amesema: "Katika mkutano wetu mkuu mwaka mmoja uliopita mjini Karlsruhe,tulishauriana na tangu wakati huo tumekuwa kila mara tukisema hali kama ile iliyoshuhudiwa mwishoni mwa msimu wa kiangazi mwaka 2015, haiwezi, haibidi na haistahiki kutokea tena. Hilo ndilo lengo langu na letu sote la kisiasa."

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef