Wamisri wamiminika vituoni kuchagua wabunge
28 Novemba 2011Wamisri wameamkia vituoni kupiga kura katika uchaguzi uliozungukwa na ghasia na mgogoro wa kisiasa. Miezi kumi baada ya kumalizika utawala wa mkono wa chuma wa miaka 30 wa Hosni Mubarak aliyeondolewa madarakani kupitia vuguvugu la kusisimua la kudai demokrasia sasa wapiga kura zaidi ya millioni 40 wanatakiwa kulichagua bunge jipya la taifa.Vijana waliojitokeza kupiga kura wanamatumaini kwamba zoezi hilo litawaletea tija na mabadiliko nchini Misri.
Kimsingi upigaji kura unafanyika kwa sehemu tatu inayoanzia hii leo katika miji mikuu ya Cairo,Alexandri na maeneo mingine lakini uchaguzi huo wenye utata utakwenda hadi mwezi Marchi na matokeo ya uchaguzi huo yatatangazwa mwishoni mwa mwezi huo. Hata hivyo ishara zinazojitokeza sio nzuri baada ya wiki nzima ya maandamano makubwa yakuutaka utawala wa mpito wa kijeshi uachie madaraka. Watu 42 waliuwawa na wengine 3000 wakajeruhiwa kufuatia ghasia hizo.Vijana waliojitokeza hii leo kupiga kura pia wanaunga mkono maandamano yanayoendelea katika uwanja wa Tahrir wakisema.
''Tunabidi kuacha maandamano kwa muda tu katika kipindi cha uchaguzi,lakini wakati huohuo tunapinga kabisa utawala wa kijeshi kwasababu tuko kama wafungwa na sasa tunataka kuchagua rais atakayetuongoza.''
Wanawake na wanaume wameonekana kupanga foleni tofauti tangu saa mbili asubuhi kwa saa za misri huku idadi ya waliojitokeza kushiriki katika uchaguzi hiyo ikitajwa kuwa ya juu kabisa.Wengi waliohojiwa wakisubiri kupiga kura wameeleza kwamba uamuzi wao wa kufika kupiga kura ni kutaka kuleta mabadiliko nchini mwao hasa ikizingatiwa ni uchaguzi wa kwanza huru na wa kidemokrasia kuwahi kufanyika nchini humo.Hali ya wasiwasi ilikuwa imetanda wiki nzima hususan hapo jana na kuenekana kuhatarisha zoezi la uchaguzi lakini mtawala wa kijeshi Field Mashal Hussein Tantawi amekaza misuli na kushikilia kauli yake kwamba uchaguzi lazima ufanyike kama ulivyopangwa hii leo na kuwataka wamisri wajitokeze.
Wakati hayo yakiendelea mapema asubuhi ya leo bomba la kusambaza mafuta kuelekea Israel limeripuliwa ikiwa ni tukio la tisa kuwahi kutokea mwaka huu.Ama kuhusu vipi bunge jipya litakavyofanya kazi na ikiwa litafaulu kuumaliza mvutano na jeshi juu ya suala la madaraka yao chini ya katiba mpya itakayoundwa mwaka ujao, inabakia kuwa kitendawili kisicho jibu.
Mwandishi: Saumu Mwasimba
Mhariri : Abdul-Rahman Mohammed