1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamisri kumchagua rais hii leo

Isaac Gamba
26 Machi 2018

 Wamisri wanapiga kura hii leo kumchagua rais katika kinyang'anyiro kinachotarajiwa kumpa ushindi  kirahisi na muhula wa pili madarakani rais wa sasa Abdel Fattah al-Sisi kutokana na kutopata ushindani mkali.

https://p.dw.com/p/2uy7o
Ägypten Präsidentschaftswahlen
Picha: Reuters/Egypt TV

Vituo vya kupigia kura vimefunguliwa mapema leo Jumatatu katika zoezi hilo la uchaguzi litakalochukua siku tatu na kwa mujibu wa Televisheni ya taifa ya nchi hiyo El-Sissi alipiga kura mjini Cairo dakika chache tu baada ya vituo kufunguliwa.

Zoezi la upigaji kura lilionekana kuendelea katika maeneo kadhaa nchini humo huku baadhi ya vituo vya upigaji kura mjini Cairo vikipambwa kwa bendera ya taifa wakati magari magari yaliyokuwa jirani yakicheza nyimbo za kizalendo.

El- Sissi mwenye umri wa miaka 63 mara kadhaa amekuwa akitoa mwito kwa wanachi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi na kuahidi uchaguzi kufanyika katika mazingira huru na haki. 

Kiasi cha maafisa wa vikosi vya usalama wapatao 250,000 wamesambazwa katika vituo 14,000 vya kupigia kura katika majimbo 27 nchini humo huku siku mbili zilizopita mripuko wa bomu ukiwaua maafisawawili wa polisi katika mji wa Alexandria mji wapili kwa ukubwa nchini Misri.

Waangalizi wa uchaguzi wanasema uchaguzi huo unaonekana kutompa ushindani mkali el-Sissi ambaye mshindani wake pekee ni mfuasi wake wa muda mrefu, Moussa Mustafa Moussa, aliyejitosa katika kinyang'anyiro hicho  wakati muda wa kurejesha fomu ukiwa unakaribia kumalizika, ingawa mwenyewe amekuwa akikanusha kuwa kibaraka wa utawala wa sasa.

Wagombea kadhaa wajizuia kujitosa kuwania urais

Awali wagombea kadhaa ama walitiwa mbaroni au waliamua kujitoa kuwania nafasi hiyo kutokana na mbinyo kutoka kwa serikali ya el- Sissi ikiwa ni pamoja na jenerali wa zamani wa jeshi Sami Annan aliyetiwa mbaroni mwezi Januari siku chache baada ya kutangaza nia yake ya kuwania urais.

Ägypten Parlamentswahlen 2015
Wapiga kura wakishiriki zoezi la uchaguzi nchini MisriPicha: Reuters/M. Abd El Ghany

Jeshi la Misri lilidai kuwa Annan alighushi nyaraka ambazo zingemuwezesha kushiriki uchaguzi huo huku msaidizi wake mkuu akishambuliwa   na watu wasiojulikana wakati Abdel-Moneim Abul Fotouh aliyewania nafasi hiyo katika uchaguzi wa mwaka 2012 alikamatwa  kutokana na kushukiwa kuwa mfuasi wa kundi la udugu wa kiisilamu lililopigwa marufuku la Muslim Brotherhood pamoja na kufanya uchochezi dhidi ya taasisi za serikali.

 Mbunge wazamani Mohammed Anwar  Sadat  na kamanda mwandamizi wazamani  wa vikosi vya anga na ambaye pia aliwania urais katika uchaguzi wa mwaka 2012 Ahmed Shafiq nao pia wamejiengua kwenye kinyanganyiro hicho.

Hata hivyo katika mahojiano kwa njia ya televisheni el Sissi amesema kukosekana kwa washindani  wa uhakika dhidi yake hakusababishwi na yeye na kuwa angependelea iwapo kungekuwa na washindani hata kumi wazuri ili wapiga kura wapate kuwa na wigo mpana wa kuchagua.

Wakati baadhi ya viongozi wa upinzani wakitoa mwito wa kususia uchaguzi huo, serikali imeongeza juhudi za kuhamasisha watu kujitokeza na kupiga kura. Mabango ya kumsifia el-Sissi yameonekana kwa wingi nchini humo huku mabango ya kumtangaza mshindani wake yakionekana kuwa machache.

El-Sissi ana matumaini kushinda uchaguzi huo na kuendeleza mageuzi yake ya kubana matumizi pamoja na hatua kali za kiusalama anazodai ni za lazima katika taifa ambalo mara nyingi linaandamwa na makundi ya kigaidi.

El-Sissi alishinda kwa karibu asilimia 97 ya kura dhidi ya mgombea wa siasa za mrengo wa kushoto Hamdeen Sabbahi katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2014 ingawa ni asilimia 37 tu ya wapiga kura waijitokeza katika uchaguzi huo uliokuwa umepangwa kufanyika kwa siku mbili na hivyo mamlaka husika kulazimika kuongeza siku moja ya ziada.

Mwandishi:  Isaac Gamba/DW/DPAE/

Mhariri: Mohammed Khelef