1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiMisri

Wamisri kuenzi utamaduni mwezi huu wa Ramadhan

28 Machi 2023

Misri inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo matatizo makubwa ya kiuchumi, lakini bado Wamisri wanaendeleza desturi ya ukarimu na hasa katika mwezi wa Ramadhan

https://p.dw.com/p/4PNgr
Ukraine Krieg -  Folgen für die Nahrungsmittelindustrie Muslime Ramadan Preise Getreide Brot
Picha: KHALED DESOUKI/AFP

Familia nyingi zinakabiliana na changamoto ya mfumuko wa bei, ambao ulifikia asilimia 32.9 mnamo mwezi Februari. Hata hivyo Wamisri walijaribu kufanya manunuzi kabla ya kuanza kwa mwezi wa Ramadhan 23 mwezi Machi kwa ajili ya mahitaji ya iftar.

Mwanzilishi wa shirika dogo la kutoa misaada katika wilaya ya al-Marg katika jiji la Cairo ambaye aliomba asitajwe majina ameelezea hali ilivyokuwa mwaka jana ambapo walikuwa wakitoa vifurushi vya chakula vipatavyo 360 kila siku lakini amesema hana uhakika kama shirika lake litafikia hata vifurushi 200 vya chakula kutokana na hali ilivyo ngumu.

Hata kabla ya mzozo wa kiuchumi unaoikumba dunia kwa sasa, kutokana na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine Misri ni miongoni mwa nchi zilizoathirika vibaya kutokana na uvamizi huo ambao umeyumbisha uagizaji wa vyakula muhimu kutoka nje ya nchi.

Kulingana na Benki ya Dunia asilimia 30 ya Wamisri wanaishi katika umasikini na idadi kama hiyo imo kwenye hatari kutumbukia katika janga la umaskini. Huku kupanda kwa gharama za chakula cha mifugo kumefanya wamisri wapatao milioni 105 kushindwa kugharamia mlo wa kuku uliokuwa unapatikana kwa bei nafuu hapo awali.

Kabla ya kuanza mwezi wa Ramadhani mashirika ya misaada yaligundua kwamba misaada ambayo mamilioni ya Wamisri wanaitegemea haitapatikana kwa urahisi na hapo mashirika hayo yaliibua hofu kwa kueleza kuwa yalikuwa yanahangaika kukidhi mahitaji ya watu zaidi wanaohitaji misaada, wakati ambapo gharama zimepanda juu, huku michango ikipungua zaidi.

Lakini utamadunni wa ukarimu, hasa wakati wa shida, unazingatiwa zaidi wakati wa mwezi wa Ramadhani ambapo Wamisri wengi wanatoa misaada kwa wingi. Kila siku ya mwezi mtukufu, sehemu kubwa katika  mitaa ya jiji la Misri wakati wa magharibi utaona meza zilizojazwa maankuli yaliyotolewa kwa hisani ambapo mamia ya watu huja kufungua na kula futari bila malipo.

Kulingana na takwimu rasmi za mwaka 2021, wastani wa mshahara wa chini ni dola 129 kwa mwezi  nchini Misri. Kwa sasa bei ya kilo moja ya nyama imeongezeka na kufikia robo ya mshahara huo. Vipato vimepungua huku sarafu ya Misri ikipoteza thamani yake kwa kiwango cha nusu na kutokana na hali hiyo watu wengi zaidi wanatatizika kupata riziki kwa ajili ya kujikimu.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Misri, wamisri walitoa misaada kufikia dola milioni 315 mnamo mwaka 2021 ambapo asilimia 90 ya misaada hiyo ilitumika katika mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Mkuu wa shirika moja linalosimamia misaada ya nguo Manal Saleh amesema utamaduni wa kutoa misaada wakati wa Ramadhan utaendelea licha ya wamisri kukumbwa na majanga hapo awali. Amesema japo watu hawana kikubwa cha kutoa lakini bado wamisri wanajitahidi kutoa misaada ya kifedha au hata kwa kujitolea kupika chakula na kuwapa wanaohitaji pale wanapokuwa hawana fedha za kutoa.

Mwandishi: Naomi William