Wamarekani wamlaumu Trump kusitishwa shughuli za serikali
28 Desemba 2018Utafiti wa shirika la habari la Reuters umedhihirisha kwamba asilimia arubaini na saba ya raia wa Marekani walioshiriki katika utafiti huo wanamlaumu Rais Trump, na asilimia 33 wanaulaumu upande wa chama cha Democratic. Asilimia saba ya raia wanawalaumu maseneta wa chama cha Republican.
Kusitishwa kwa shughuli za serikali ya Marekani kumetokana na madai ya Rais Trump ya kutaka apatiwe dola bilioni tano za walipa kodi, ili ajenge ukuta katika mpaka wa Marekani na Mexico . Lengo la Trump la kujenga ukuta huo ni kuzuwia wahamiaji kuingia nchini Marekani. Madai hayo ya Trump yamepingwa vikali na maseneta wa chama cha Democratic na baadhi kutoka chama chake cha Republican. Gharama jumla ya ujenzi wa ukuta huo inakadiriwa kuwa dola bilioni 23.
Ikiwa takriban wiki nzima imeshapita, hali hiyo imeanza kuathiri maelfu ya wafanyakazi wa serikali pamoja na raia wa kawaida wanaotegemea huduma za umma. Miongoni mwa shughuli zilizokwama ni: serikali haiwezi kutoa sera mpya za bima ya mafuriko na mjini New York jaji mkuu wa mahakama za shirikisho za Manhattan amesitisha kazi kuhusu kesi za kiraia zinazohusisha wanasheria wa serikali ya Marekani, ikiwa ni pamoja na kesi kadhaa ambazo Rais Donald Trump mwenyewe ni mshtakiwa.
Baraza la Wawakilishi kufanya uamuzi
Baraza la Congress limeahirishwa wiki hii bila ya mafanikio yoyote juu ya suala hilo, huku Trump akilazimisha apatiwe fedha anazozihitaji kujenga ukuta huo na wabunge wa chama cha Democratic wakiendelea kukataa kumpa anachokitaka.
Kiongozi wa upande wa Democratic Nancy Pelosi katika Baraza la Wawakilishi amesema, ikiwa hadi Januari 3 Baraza la Seneti litashindwa kuafikiana juu ya mswada huo basi Baraza la Wawakilishi litafanya uamuzi.
Lakini hata hilo litakuwa vigumu kufanikishwa kwasababu Baraza la Seneti bado linahodhiwa na chama cha Republican, na saini ya Trump itahitajika kupitisha mswada wowote ule na kuwa sheria.
Majadiliano yanaendelea kati ya upande wa Republican na Democratic, lakini hamna kubwa ambao Baraza la Seneti linaweza kuamua bila ya rais wa nchi hiyo.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap,rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga