wamarekani waliouwwa Iraq
30 Julai 2008Idadi ya wanajeshi wa kimarekani waliouwawa vitani nchini Irak hadi sasa mwezi huu ,imepungua mno Julai hii inayomalizika na idadi jumla ya kila mwezi, yamkini ikawa ya chini sana tangu Marekani kuongoza uvamizi wa Iraq 2003.
►◄
Wanajeshi 5 wa kimarekani wameuwawa katika mapigano mwezi huu wa Julai unaomalizika leo ukilinganisha na 66 mwezi kama huu mwaka jana.hii ni kwa muujibu wa mtandao huru Icasualties.org unaoweka rekodi za maafa yanayowsapata wanajeshi wa Marekani katika vita hivi.
Kupungua huko kunathibitisha zaidi kuteremka mno kwa machafuko nchini Iraq kwa kiwango ambacho hakijaonekana tangu mapema 2004.
Wakitegemea hali hii, maalfu ya askari wa kiiraki walianza mapambano makali katika mkoa wa kaskazini-mashariki wa Diyala hapo jana.
kikundi cha wapiganaji wa Al qaeda kikijaribu kuchochea machafuko huko Diyala ambako kuna mchanganyiko wa madhehebu ya kidini na si mbali sana na mji mkuu Baghdad.
Msemaji wa wizara ya ulinzi Meja-jenerali Mohammed -Askari amearifu hapo jana kwamba wafuasi 35 wenye siasa kali wametiwa kizuizini hadi sasa.Polisi wa Irak pamoja na vikosi 2 vya jeshi la Iraq kila moja kikiwa na kiasi cha askari 9,000 wanashiriki katika msako huo.
Kupelekwa vikosi zaidi vya Marekani nchini Iraq mwaka jana, uamuzi wa viongozi wa makabila ya kiarabu kuwageukia Al qaeda na kusimamishwa mapigano kuliko amrishwa na kiongozi wa madhehebu ya shia Moqtada al-Sadr kwa jeshi lake la Mehdi, ndiko kulikochangia hali hii ya kupungua kwa machafuko.
Idadi ya askari wa Marekani waliouwawa katika vita mwezi huu wa Julai imepungua kutoka 23 mwezi uliopita wa Juni na 15 hapo Mei.
Kwa jumla, askari 9 wameuwawa mwezi huu wa julai wale mapiganoni na wengine katka shughuli nyengine.
Wizara ya ulinzi ya Marekani imetangaza pia kuwa mwezi huu imezitambua maiti za wanajeshi wake 2 walionyakuliwa Mei mwaka jana.
Wanajeshi jumla wa Marekani waliouwawa katika mapigano na nje ya mapigano Juni mwaka huu ilikua 29 na mwezi Mei ilikua 19.
Idadi hii inatofautiana sana na ile katika vita nchini Afghanistan ambako askari zaidi wa kimarekani waliuliwa hapo Mei na juni mwaka huu ukilinganisha na ile nchini Iraq.
Kuna askari 144,000 wa kimarekani nchini Iraq na 36,000 nchini Afghanistan.
Kiasi cha askari 4,120 wa kimarekani wameuwawa nchini Iraq tangu kuvamiwa Irak.Idadi huko Afghanistan ni 561 tangu pale utawala wa wataliban ulipoangushwa 2001.