Waliouwawa shambulio la Yemen ni zaidi ya 80
22 Januari 2022Ofisi ya habari ya waasi wa Houthi imeripoti idadi hiyo ya vifo ikiendelea kusema kuwa, bado waokoaji wanaendelea kuwatafuta majeruhi na mabaki ya miili ya watu wengine wanaohofiwa kufa kwenye eneo la gereza hilo kaskazini mwa Saada mpakani na Saudi Arabia.
Tukio hilo la Ijumaa ni sehemu ya mashambulizi ya angani na ardhini yanayozidi kuchochea mzozo wa Yemen yenye vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa miaka kadhaa.
Katika hatua nyingine, shirika la habari la SPA la Saudi limeripoti kuwa, muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi kupitia kwa msemaji wake umesema, ripoti kwamba wameshambulia gereza hilo siyo za kweli na kwamba wataijulisha ofisi ya masuala ya haki za binadamu ya Yemen pamoja na kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu kuhusu ukweli na taarifa zaidi.
Shambulio hilo limeibua ukosoaji wa muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia kutoka kwa Umoja wa Mataifa. mashirika ya misaada ya kimataifa na makundi ya kutetea haki za binadamu.
Kwa mujibu wa shirika la hisani la madaktari wasio na mipaka , karibu watu 200, walijeruhiwa katika shambulio hilo la anga lililofanywa jana Ijumaa.
Waasi wadaiwa kutumia udanganyifu kwenye mzozo
Msemaji wa muungano huo wa kijeshi Brigedia Jenerali Turki al-Malki amewatuhumu waasi wa Houthi kuwa hawakutoa taarifa kwa kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu kuwa eneo la gereza lililolipuliwa ni moja ya sehemu zinazohitaji ulinzi dhidi ya mashambulizi ya anga. Amedai kuwa, kushindwa kwa waasi hao kufanya hivyo kunaakisi kawaida ya wapiganaji hao ya kutumia njia za udanganyifu katika mzozo huo.
Waasi wa Houthi walikuwa wakitumia gereza lililoshambuliwa kuwashikilia wahamiaji waliokamatwa wengi wao wakiwa ni Waafrika waliokuwa wakijaribu kuelekea Saudi Arabia kupitia Yemen.
Mzozo katika taifa hilo masikini la kiarabu ulianza mwaka 2014 waasi wa Houthi walipoudhibiti mji mkuu Sanaa na sehemu kubwa ya kaskazini mwa Yemen na hivyo kuilazimu serikali kukimbilia kusini na kisha uhamishoni nchini Saudi Arabia.
Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia, wakati huo ukiungwa mkono na Marekani, uliingia vitani miezi kadhaa baadaye katika jaribio la kuirejesha serikali madarakani. Mgogoro huo umekuwa moja kati ya mizozo mibaya zaidi ya kiutu duniani huku jumuiya ya kimataifa ikikosoa mashambulizi ya anga ya Saudia ambayo yamewauwa mamia ya raia na kuharibu miundo mbinu ya serikali. Waasi wa Houthi kwa upande wao wamekuwa wakiwatumia watoto kama sehemu ya wapiganaji wao na kuweka mabomu ya ardhini kote nchini humo