1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Walioambukizwa corona Ujerumani wafika milioni moja

27 Novemba 2020

Ujerumani imefikisha idadi ya watu milioni moja walioambukizwa virusi vya corona huku wataalamu wa Marekani wakihofia sherehe za kutoa shukrani maarufu kama 'Thanks giving' huenda zikasababisha watu zaidi kuambukizwa.

https://p.dw.com/p/3luId
Deutschland | Weihnachten in der Coronakrise 2020
Picha: Ying Tang/NurPhoto/picture alliance

Kulingana na Idadi ya maambukizo iliyotolewa na chuo kikuu cha Marekani cha Johns Hopkins, Ujerumani mpaka sasa ina zaidi ya watu milioni moja waliambukizwa virusi vya corona. Hali hiyo imefikiwa baada ya taasisi za afya nchini humo kurekodi maambukizi mengine mapya 22,268 jana Alhamisi na vifo 389. Kwa Ujumla watu 15,160 wameshafariki kutokana na ugonjwa wa COVID 19 nchini Ujerumani.

Ujerumani imeongeza muda wa masharti au vizuizi vya kudhibiti virusi hivyo hadi mwishoni mwa mwezi Desemba. Kansela wa nchi hiyoAngela Merkel ametetea uamuzi wake na wa viongozi wa majimbo 16 ya Ujerumani juu ya kurefusha muda huo akisema kuwa mikakati inayochukuliwa kwa sasa imefanikiwa kwa kiasi fulani kudhibiti maambukizi zaidi ya virusi vya corona. 

Akilihutubia bunge la Ujerumani hapo jana Merkel amesema juhudi zaidi zinapaswa kufanywa ili kukwepa kuuwekea mzigo mfumo wa afya wa Ujerumani. 

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel
Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Felix Zahn/imago images/photothek

Huenda maambukizi zaidi yakatokea Marekani kutokana na sherehe za "Thanksgiving"

Nchini Marekani, raia wa taifa hilo walioshiriki sherehe za kushukuru au Thanks giving walitakiwa kuepuka kujiunga na mikusanyiko mikubwa ya watu ili kupunguza kusambaa kwa virusi vya corona vilivyosababisha vifo vya watu  260,000 nchini humo.

Familia nyingi ziliishia kuonana mitandaoni huku zikiendelea na mlo wao wa jioni wa sherehe hizo za Thanks giving.

Soma pia: Corona yaendelea kulisakama bara la Ulaya na Marekani

Lakini taasisi ya usalama wa usafiri wa Marekani imeripoti wasafiri milioni 6 waliopitia viwanja vya ndege  vya Marekani kati ya Ijumaa na Jumatano wiki hii na kuvifanya viwanja hivyo kuwa na shughuli nyingi tangu kuanza kwa corona mwezi Machi. Wataalamu wa afya hata hivyo wana wasiwasi kuwa muhula wa mapumziko huenda ukasababisha kuongezeka kwa maambukizi zaidi Marekani. 

Hali barani Ulaya nako sio ya kuridhisha mwanamfalme wa Sweden Carl Philip na mke wake Sophia kwa sasa wapo karantini baada ya kuambukizwa corona. Familia hiyo kwa sasa ipo salama na inaendelea vizuri hii ikiwa ni kulingana na taarifa kutoka ikulu ya kifalme. 

Wahudumu wa afya wakimhudumia mgonjwa hospitalini mjini Naples Italia. 19.11.2020
Wahudumu wa afya wakimhudumia mgonjwa hospitalini mjini Naples Italia. 19.11.2020Picha: Fotogramma/IPA/ABACA/picture alliance

Hungary kwa upande wake haina mipango ya kuanzisha mikakati mapya ya kudhibiti virusi hivyo hii ikiwa ni kulingana na mnadhimu wa Waziri Mkuu Viktor Orban, Gergely Gulyas licha ya maafisa wa afya kuripoti vifo na maambukizi kadhaa ya corona.  Gulyas lakini amesema hali itatathminiwa tena wiki ijayo. 

Mataifa zaidi yachukua juhudi za kudhibiti ugonjwa wa COVID 19

Upande wa Asia Korea Kusini imerekodi, zaidi ya maambukizi mapya 500 ya ugonjwa wa COVID 19 kwa mara ya kwanza baada ya takriban miezi minane. 

Shirika la kudhibiti magonjwa ya kuambukiza nchini humo limesema visa 583 ndani ya masaa 24 iliyopita imefikisha idadi jumla ya walioambukizwa kufikia 32,318, huku watu  515 wakifariki.

Korea Kusini imekuwa na ongezeko kubwa la maambukizi tangu ilipolegeza masharti ya kukabiliana na virusi hivyo. na kwa sasa wameweka masharti mapya ya kudhiti hali. 

Barani Afrika hali sio tofauti sana, na mataifa mbali mbali yanaendelea kuchukua tahadhari ya kudhiti kusambaa zaidi kwa virusi ivyo vya corona. 

Vyanzo: jsi/rt (AP, dpa, AFP, Reuters)